WIZI WA MITIHANI NI SAWA NA UHUJUMU UCHUMI -PROF.MKENDA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, February 8, 2023

WIZI WA MITIHANI NI SAWA NA UHUJUMU UCHUMI -PROF.MKENDA


Na Okuly Julius-Dodoma

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ametoa ufafanuzi juu ya wanafunzi 337 ambao matokeo yao ya kidato cha nne mwaka 2022 yamezuiliwa na Baraza la Mitihani la Tanzania kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo wizi wa mitihani na udanganyifu.

Prof Mkenda ametoa ufafanuzi huo leo Februari 8,2023 mbele ya waandishi wa habari ,kufuatia Video iliyosambaa mitandaoni ikionesha Wazazi wa wanafunzi waliosoma shule ya Sekondari Thaqaafa iliyopo Jijini Mwanza wakiandamana kudai Watoto wao hawajatolewa matokeo ya Kidato Cha Nne.

"Kati ya watahiniwa 560375 waliofanya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2022 matokeo ya watahiniwa 337 sawa na asilimia 0.06 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani wamefutiwa matokeao kwa makosa mbalimbali ikiwemo kujaza matusi,kuingia kwenye chumba cha mitihani na maandishi,kuingia na simu na smartwatch,"amesema Prof.Mkenda 


Mkenda amechanganua makosa hayo kuwa watahiniwa 4 waliandika matusi,51 waliingia na maandishi katika vyumba vya mtihani,10 waliingia na simu na smartwatch,watahiniwa 9 hawakwenda kabisa kufanya mitihani badala yake walifanyiwa na watu wengine.

Watahiniwa wengine ni watahiniwa 20 walikamatwa wakifundishwa,6 walikamatwa wakitumia jukwaa la WhatsApp kujibu mtihani,20 matokeo yao yamezuiwa wakati wanafunzi 206 wamefutiwa mtihani kutokana na matokeo yao kufanana kusiko kawaida.
 
Ambapo kati ya wanafunzi 206 kuna wanafunzi 140 kutoka shule ya Thaqaafa ya Jijini Mwanza na wanafunzi 66 kutoka shule ya Twibhoki Serengeti , mkoani Mara na mpaka sasa watuhumiwa 12 wapo mahabusu kutokana na makosa hayo.


" Wizi wa Mitihani ni kosa kubwa sana ni sawa na uhujumu uchumi na hatakubaliana nalo na wezi wa mitihani lazima wakamatwe na washughulikie kisheria kwa sababu haivumiliki,"

Na kuongeza kuwa ‘’Dawa ya kwanza ya Mwalimu anayevujisha mitihani ni kufutwa Kazi na kufunguliwa mashitaka kwani gharama ya kurudia mtihani ni kubwa sana na inatumia fedha nyingi za kodi ya watanzania kurudia mitihani,"amesisitiza Mkenda

Waziri huyo amefafanua kuwa tayari barua zimeandikwa kwa Mamlaka husika juu ya Wasimamizi wa mitihani hiyo kwani Kuna uchunguzi unaonesha Usimamizi ulikuwa Mbovu huku Polisi wakiendelea kufanya uchunguzi, kwa kuhoji wanafunzi na Walimu ambapo wanafunzi wamekiri.

Prof.Mkenda amesema kuwa Wizara imeridhika hatua ambazo Baraza la Mitihani la Tanzania limechukua na Kuna Sheria zinakuja ambazo zitaruhusu Hatua Kali zaidi kuchukuliwa kwa wanaofanya udanganyifu wa mitihani.

No comments:

Post a Comment