Na OR-TAMISEMI
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ikiongozwa na na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Stanslaus Mabula (Mb) imekagua na kuridhishwa na matumizi ya fedha na usimamizi wa Ujenzi wa Kituo cha Afya Kasekese kilichojengwa wilayani Tanganyika Mkoani Katavi.
Hayo yameelezwa tarehe 21 Machi 2023 na Makamu Mwenyekiti wa Kamati wakati Kamati ya LAAC ilipoambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange kukagua ujenzi wa kituo hicho.
“Kamati imeridhishwa na kazi iliyofanyika katika mradi tuliotembelea wa Kituo cha Afya Kasekese na niwape hongera mafundi waliofanya kazi hii wamefanya kazi kwa uzalendo wa hali ya juu” amesema Mabula
Aidha, Kamati imepongeza Halmashauri kwa kusimamia kikamilifu fedha zilizotolewa na Serikali kuboresha huduma za afya katika kituo cha afya Kasekese ambapo awali ilikuwa Zahanati.
Kamati imeelekeza kukamilishwa kwa nyumba ya Mtumishi wa kituo cha Afya ikiwa ni pamoja na Kuunganisha umeme na kumalizia kazi ndogo ndogo za Ukamilishaji wa nyumba hiyo ambayo imeshaanza kutumika.
Kituo cha Afya Kasekese Kimeshaanza kutoa huduma za Wagonjwa wa nje katika Jengo la OPD liliojengwa kwa kupitia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ambapo Majengo Mengine yapo katika hata za Ukamilishaji.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya hesabu za Serikali za Mitaa inaendelea na ziara ya kukagua miradi ya Maendeleo katika Sekta za Elimu, Afya na Vikundi vya akina Mama, Vijana na Watu Wenye Ulemavu katika Halmashauri za Mkoa wa Katavi.






No comments:
Post a Comment