DKT.JAFO ASISITIZA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KWA SHULE NA TAASISI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, April 27, 2023

DKT.JAFO ASISITIZA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KWA SHULE NA TAASISI.


Na Mwandishi wetu Iringa 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesisitiza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa shule na taasisi ili kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.


Amesema hayo leo Aprili 27, 2023 wakati akizungumza na wanafunzi, walimu na wazazi wakati wa mahafali ya wahitimu wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Iringa.


Dkt. Jafo amesisitiza katazo la matumizi ya kuni na mkaa lililotolewa na Serikali hivi karibuni haliwahusu watumiaji wadogo bali kwa taasisi zinazolisha watu kuanzia 100 na kuendelea.



Amesema ekari za miti zinapotea kwa kukatwa na ndio maana Serikali inasimamia kampeni mbalimbali za upandaji wa miti kote nchini ikiwemo ‘Kampeni ya Soma na Mti’ ili kukabiliana na changamoto za kimazingira.


Amesema katika kuunga mkono hatua hiyo Kampuni ya Gesi ya Taifa inatarajia kufunga mtungi wa nishati hiyo katika Shule ya Wasichana ya Iringa hatua itakayosaidia kusitisha matumizi ya kuni.



“Tuna dhamana ya utunzaji mazingira kwa kuacha kukata miti ,ndio maana nilitoa maelekezo kuhusu matumizi ya nishati safi kwani matumizi ya gesi huokoa fedha ambazo zinatumika kwa ajili ya kuni na mkaa kwa ambazo ni shilingi milioni tano hadi nane kwa mwezi.


“Ukiangalia katika matumizi ya gesi kwa mwezi tani moja ni shilingi milioni mbili kule katika Shule ys Sekondari Ruvu nilikuwepo juzi wameanza kutumia gesi na kuachana na matumizi ya kuni sasa lengo letu itafikia muda tutaacha kabisa kutumia kuni,” amesisitiza.



Dkt. Jafo ameipongeza Jumuiya ya shule hiyo kwa upandaji wa miti kusema kuwa iwe ya mfano kwa shule zingine nchi ili kusukuma mbele ajenda ya utunzaji wa mazingira inayosisitizwa na viongozi wa Serikali.



Pia, amewataka wahitimu hao na wanafunzi kwa ujumla kutojihusisha na vitendo vinavyoenda kinyume cha maadili kwani vitawaharibia maisha yao hivyo kuharibu ndoto zao.

No comments:

Post a Comment