Na WAF, Bungeni Dodoma.
NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa kundi la wafungwa ni moja kati ya makundi maalumu ambayo Serikali imeliweka kwenye wanufaika wa mpango wa Bima ya Afya kwa wote, huku akiweka wazi kuwa, kwasasa Serikali imeweka utaratibu maalum wa kutoa huduma za matibabu kwa wafungwa katika magereza mbalimbali nchini kupitia vituo vya kutolea huduma za Afya vya serikali bila malipo.
Dkt. Mollel amesema hayo, leo Aprili 19, 2023 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Mhe. Asia Halamga katika Mkutano wa kumi na moja kikao cha kumi.
"Katika kuhakikisha kuwa wafungwa wanapata haki yao ya msingi ya kupata huduma za afya, Serikali imeweka utaratibu maalum wa kutoa huduma za matibabu kwa wafungwa katika magereza mbalimbali nchini kupitia vituo vya kutolea huduma za Afya vya serikali bila malipo yoyote." Amesema
"Serikali inakamilisha Muswada wa bima ya Afya kwa wote ambapo utakapokamilika utakuwa suluhisho ya upatikanaji wa huduma za afya kwa makundi yote ya kijamii wakiwemo wafungwa." Amesisitiza Dkt. Mollel.
Aidha, Dkt. Mollel amesema, katika vituo vya kutolea huduma za afya vyote kuna Wataalamu wa ustawi wa jamii ambao kazi yao kubwa ni kuhakikisha watu wenye uhitaji wakiweni wenye ulemavu wanapata huduma za matibabu kulingana na vigezo.
Kwa upande mwingine, Dkt. Mollel ameeleza katika kudhibiti matumizi holela ya dawa za binadamu, Serikali imekuwa ikitoa elimu kupitia vyombo vya habari, kusimamia mwongozo unaobainisha matibabu kwa kila ugonjwa ikiwemo dawa zinazohitajika kutibu magonjwa hayo na kusimamia ueledi wa watoa dawa katika maeneo yote yanayohusika na utoaji wa dawa kama vile maduka ya dawa na vituo vya kutolea huduma za afya.
Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema, Wizara kwa kushirikiana na OR TAMISEMI itaendelea kutafuta vibali vya ajira kwaajili ya kuajiri wafamasia ili kutatua changamoto ya uhaba wa wafamasia nchini utaosaidia kupunguza changamoto ya matumizi holela ya dawa.
Pamoja na hayo, Dkt. Mollel amesema, Serikali itaendelea kusimamia vizuri na kuhakikisha utaratibu unafuatwa na wafanyabiashara ili kuzilinda afya za wananchi.
No comments:
Post a Comment