Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula amesema hayuko tayari kuona madudu yanayoendelea katika Jiji la Dodoma kutokana na vitendo vya ubadhilifu vinavyoendelea katika Sekta ardhi Jiji la Dodoma.
Waziri Mabula alibainisha kuwa kuna baadhi ya watendaji ambao wamekuwa wakirubuni wananchi kwa kuwaidai hongo ili waweze kuwapatia namba ya malipo (control number) na kuonya kwanini mwananchi anunue haki yake jambo ambalo ni kinyume na maadili.
Waziri Mabula amebainisha hayo wakati wa ufunguzi wa Kikao kazi kilichowakutanisha Watendaji Sekta ya Ardhi pamoja na makampuni ya Upimaji katika Mkoa wa Dodoma mapema jana Jijini Dodoma.
Dkt. Mabula pia ameonesha kutoridhishwa kwake na huduma inayotolewa na vijana wenye ajira za kujitolea ambao amedai kuwa wamekuwa sio weledi katika utoaji huduma za ardhi kwa wananchi na kuonya kuwa mapungufu yaliyopo katika sekta ya ardhi Jijini Dodoma yanatokana na uwepo wa vijana hao ambao uchunguzi wa awali unaonesha wanamiliki mali nyingi.
Kufuatia hali hiyo Dkt. Mabula tayari amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kufuta mikataba ya vijana hao ambao kwa kiasi kikubwa wana mmomonyoko wa maadili na wamekuwa chanzo cha migogoro ya ardhi.
Dkt. Mabula alibainisha kuwa katika Halmashauri ya Jiji Dodoma kuna Vijana wengi wanaojitolea na hawalipwi na mamlaka hiyo akihoji namna ambayo wamekuwa wakijipatia kipato bila kuwa na malipo kutoka taasisi yoyote.
Dkt. Mabula alioneshwa kushangazwa na kitendo cha vijana hao kugomea kazi za muda mfupi katika mradi mpya wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi unaoendelea sehemu mbalimbali wakidai malipo ya elfu sitini kwa siku hayatoshi.
Ni mazingira haya yanayomsukuma Kiongozi huyo wa Wizara Kwenda mbali zaidi kumtaka Mkurugenzi wa Jiji Dodoma kuangalia upya vigezo vya ajira ya mkataba laikini pia kuwataka vijana hao kukabidhi ofisi na kama kuna miradi ambayo wanaisimamia waikabidhi haraka.
“Ni wapi Vijana hawa wanapata fedha nyingi na wanamiliki vitu vyenye thamani ikiwemo magari na nyumba sio kula rushwa, wakiambiwa kuhusu kuajiriwa hawataki na hata tulijaribu kuwapa ajira ya muda katika mradi uliotayari kuwapa malipo ya elfu sitini kwa siku hawakuwa tayari kwa madai kuwa malipo ni madogo”. Alihoji Waziri Mabula.
Dkt. Mabula amebaini kuwepo kwa watumishi wasiokuwa waadilifu wanaokiuka mpango kina uliopo na kudiriki kugawa viwanja katika eneo la makaburi na sehemu ya kingo za mto ili kugawia wananchi maeneo hatarishi akitaja tabia hiyo kama tamaa isiyofaa.
No comments:
Post a Comment