Na Okuly Julius- Bahi,Dodoma
Akizungumza Mei 7,2023 katika Kijiji cha Maya Maya Wilayani Bahi Mkoani Dodoma,Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe,Dkt.Dorothy Gwajima amesema changamoto kubwa dhidi ya ukatili wa watoto ni ukimya na kumalizana miongoni mwa wanafamilia na matokeo yake taarifa hazifikishwi kwenye vyombo vya sheria.
"Wazazi tumeacha njia ya malezi kwa watoto wetu ndio maana vitendo vingi vya ukatili dhidi ya watoto vinaripotiwa kutokea nyumbani hii ni kwa sababu tumewaacha watoto wajilee wenyewe na hapo ndio wanashawishika na kuingizwa kwenye mitego ya kubakwa na kulawitiwa,"
Na kuongeza kuwa "mfano kwa mujibu wa taarifa ya polisi kuanzia Januari hadi Desemba mwaka 2022 matukio ya ukatili dhidi ya watoto yaliyoripotiwa yalikuwa ni 12,163 ambapo wasichana ni 9,962 na wavulana ni 2,201 ukilinganisha na matukio ya 2021 ambapo yalikuwa 11,499 utagundua hapo kuna ongezeko la matukio 664 sawa na asilimia 5.8,"amesema Dkt.Gwajima
Aidha ,Dkt.Gwajima amebainisha kuwa matukio yaliyoongoza ni ubakaji 6,335,ulawiti 1,557 na mimba za utotoni 1,557 ambapo Mikoa iliyotoa takwimu kubwa ni Arusha matukio 728,Mbeya 710,Kinondoni 681,Tanga 607 , na Mwanza matukio 595 na hii imechangiwa na uimara wa mifumo katika kuelimisha jamii iwe na uthubutu wa kutoa taarifa badala ya kuficha.
Pia ,Dkt.Gwajima amesema kuwa wakati wa kuoneana aibu na kuacha adui kushambulia watoto umepitwa na wakati hivyo jamii ivunje ukimya na kuondoa aibu katika kuripoti matukio ya ukatili kwa watoto kwani watu katili hutumia faida ya aibu na ukimya kuteka fahamu za watoto.
Waziri huyo ametoa wito kwa familia kutumia siku hiyo kujadili changamoto na kutafuta masuluhisho na majawabu ya namna ya kendeleza amani na upendo ili kudumisha mshikamano katika familia na jamii kwa ujumla.
Pia amewataka viongozi wa Mikoa na Halmashauri kuhusika kikamilifu katika maandalizi ya siku hiyo na sio tu kwa kushirikisha viongozi wa serikali bali watu wa kawaida yaani jamii wakiwemo viongozi wao wa dini,mila,wazazi,walezi na watoto wenyewe ili wahusike katika mjadala ya malezi na makuzi ya watoto na mmomonyoko wa maadili unaoendelelea katika jamii.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bahi Godwin Gondwe amesema kuwa Wilaya yake inaungana moja kwa moja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii kupinga na kutokomeza kabisa ukatili dhidi ya watoto kwani bila kufanya hivyo taifa la baadae litapoteza nguvu kazi.
"Wilaya ya Bahi tupo kivitendo zaidi na ndio maana tumenzisha vilabu vya kupinga ukatili dhidi ya watoto kwanzia ngazi ya wilaya mapaka familia tunahamasishana umuhimu wa kuwalinda watoto kuanzia nyumbani hivyo nakuahidi Waziri tupo pamoja katika mapambano haya,"amesema Gondwe
Maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Familia Duniani kwa mwaka huu wa 2023 yanabebwa na kauli mbiu isemayo "Imarisha Maadili na Upendo kwa Familia Imara" yatafanyika katika ngazi zote kwa maana ya kila Mkoa mpaka ngazi ya familia.
No comments:
Post a Comment