Na Okuly Julius-Dodoma
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeliomba Bunge kuidhinisha jumla ya Shilingi Trilioni 1.67 kwa ajili ya makadirio ya matumizi ya wizara hiyo kwa Mwaka wa fedha wa 2023/24.
Ambapo akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo leo Mei 16,2023 Bungeni Jijini Dodoma Prof.Adolf Mkenda ametaja Vipaumbele vya Wizara kwa mwaka wa fedha 2023/24 kuwa ni kukamilisha mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mitaala ya Elimu na kuanza utekelezaji, kuongeza fursa na ubora wa mafunzo ya amali (Ufundi) katika elimu ya sekondari na vyuo vya Kati vya Amali, kuongeza fursa na ubora wa Elimu ya Msingi na Sekondari, kuongeza fursa na ubora wa Elimu ya Juu na kuimarisha uwezo wa nchi katika Utafiti, Matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ili kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Pia Prof.Mkenda amesema ,Serikali itawezesha ukarabati shule za sekondari za ufundi na kuzipatia vifaa vya kujifunzia na kufundishia; Aidha, itaendelea kukiwezesha Chuo cha Ualimu Kleruu na Mtwara Ufundi kuendelea kutoa mafunzo ya ualimu wa ufundi kwa lengo la kuongeza walimu wa ufundi nchini pia, itaboresha vyuo vya ualimu 10 ikiwa ni pamoja na chuo cha ualimu Mtwara Kawaida na Mtwara ufundi na kuwawezesha walimu tarajali kupata mafunzo ya Shahada ya Amali kwa kutumia wahitimu wa Vyuo vya Ufundi (TET) na Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VET).
Pia,Serikali itajenga karakana 10 na kuweka mitambo na vifaa katika vyuo vya ualimu ambavyo kwa lengo la kuimarisha utoaji wa mafunzo ya elimu ya ufundi kwa vitendo.
Aidha, itaongeza udahili wa wanafunzi katika vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi kutoka 51,382 hadi 66,459 wakiwemo 5,000 kutoka kwenye mazingira magumu 1,500 wenye mahitaji maalum na wajasiriamali 2,000 watakaopatiwa mafunzo kupitia programu ya INTEP.
Pamoja na hayo ,Serikali itadahili wanafunzi 660 katika Chuo cha Ualimu wa Mafunzo ya Ufundi Stadi Morogoro – MVTTC kwa lengo la kuongeza idadi ya walimu wanaofundisha katika Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Vyuo vya Ualimu wa Mafunzo ya Ufundi na tatoa ithibati kwa vyuo 70 vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kwa lengo la kuwezesha vyuo kukidhi viwango vya utoaji wa elimu bora.
Pia ,Serikali itasajili shule za msingi na sekondari takribani 560 za awali, awali na msingi 380, sekondari 165, chuo cha ualimu kimoja cha binafsi na nyingine kwa kuzingatia maombi yatakayowasilishwa na kukidhi vigezo.
Prof.Mkenda amesema kuwa ,Serikali itaanza kusajili shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu kwa mfumo wa kielektroniki kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuwafikia wadau wengi zaidi. Pia, itanunua magari 12 na kuweka samani katika ofisi 195 za uthibiti ubora wa shule kwa lengo la kuboresha mazingira ya utendaji wa kazi.
Aidha ,Serikali itaongeza fursa za mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu kutoka 202,877 hadi 210,169, itaendelea kusajili wanafunzi 72,361 wa mwaka wa kwanza katika mfumo wa malipo wa kidijitali (DIDiS) na itaboresha mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Mikopo na utunzaji wa nyaraka (iLMS, MUSE, DIDis) Gateway, OLAMS, MEL na eDMS kuwa wenye ufanisi na tija.
Serikali itaendelea kutoa fursa za Elimu ya Juu kwa wanafunzi wenye ufaulu uliojipambanua kutoka wanafunzi 593 hadi 1200 kupitia Samia Skolashipu na itajenga kampasi 14 za vyuo vikuu katika mikoa ambayo haina kwa lengo la kuleta mageuzi ya kiuchumi.
No comments:
Post a Comment