Na. Samwel Mtuwa , Dodoma
Wataalam wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na mwakilishi kutoka Taasisi ya Jiolojia ya China (CGS) leo tarehe 12/6/2023 wamekutana jijini Dodoma kwa ajili ya majadiliano juu ya namna bora ya kuendeleza ushirikiano wa kikazi katika maeneo mbalimbali ikiwemo kufanya tafiti za kina za madini katika maeneo yanayoashiria uwepo wa madini pamoja kuendeleza utalii wa jiolojia nchini.
Akizungumza katika majadiliano hayo mjiolojia Junping Re kutoka CGS amewasilisha taarifa za utafiti wa madini katika mataifa mbalimbali zilizofanywa na CGS ndani ya bara la Afrika katika nchi washirika ikiwemo Tanzania.
Akifafanua katika ushirikiano huo Junping alieleza kuwa sambamba na utafiti katika madini CGS pia itaendeleza ushirikiano katika kuibua na kukuza vivutio vya utalii wa jiolojia katika maeneo yaliyoainishwa na GST kwa lengo la kuyatunza , kuyaboresha na kuyatangaza kimataifa.
Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa GST Maswi Solomon alisema kuwa kwa kipindi kirefu GST imekuwa ikifanya tafiti na kugundua vivutio vipya vya utalii wa jiolojia ikiwa pamoja na kuchora ramani inayoonesha vivutio hivyo.
Akifafanua juu ya ushirikiano wa tafiti za madini Maswi alisema kuwa CGS na GST zimekuwa zikifanya ushirikiano katika utafiti ambapo mwaka 2016 mpaka 2018 zilishirikiana katika utafiti wa Jiokemia na kutoa chapisho la Atlas ya Jiokemia (Geochemical Atlas of Tanzania) na hivyo kuongeza kuwa hatua ya sasa ni kwenda utafiti wa kina wa jiokemia kwenye maeneo yaliyotambuliwa kwenye utafiti wa awali ili kuja na taarifa za kina zinazowezesha kuvutia uwekezaji katika maeneo hayo.
Aidha, Maswi asisitiza CGS kushirikiana na GST katika kuratibu majanga ya asili ya jiolojia ikiwemo matetemeko ya ardhi ambapo CGS wamepanga kusimika kituo cha kuratibu mienendo ya mitetemo katika Mlima wa Oldoinyo Lengai mwishoni mwa mwaka huu, na hivyo kuwaomba kushirikiana na GST kwa kuwa ndio Taasisi yenye mamlaka ya kuratibu majanga ya asili ya jiolojia.
No comments:
Post a Comment