Na WMJJWM, Dar es Salaam
Serikali imesema itaendelea kushirikiana na taasisi inayosimamia utoaji wa huduma za Msimbomilia na Ufuatiliki GS1 Tanzania kuweka utaratibu wa kuchangia kuwawezesha wanawake wajasiriamali
ili kujikwamua kiuchumi kwa kuzipatia bidhaa wanazozalisha Barcodes.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa maonesho ya wiki ya Msimbomilia kwenye viwanda Juni 17, 2023 jijini Dar es Salaam.
Waziri Gwajima amesema kutokana na umuhimu wa msimbomilia ikiwemo kufanya bidhaa kutambulika kimataifa na kuingia kwenye maduka madogo na makubwa Serikali iliamua kusimamia na kushiriki katika mchakato wa kuanzishwa kwa taasisi itakayosimamia kisheria utoaji wa huduma za Msimbomilia na Ufuatiliki katika bidhaa zinazozalishwa nchini na nje ya nchi, kwani awali kulikuwa na changamoto ya bidhaa zinazozalishwa nchini kukosa utambuzi katika mifumo ya kimataifa ya Kidigitali.
"Nafurahi kusikia kuwa GS1 Tanzania imeanza kuchukua hatua za dhati za kuhakikisha kuwa bidhaa za Kitanzania pia zinaweza kuingia kwenye Maduka Makubwa ya Kisasa kwa
kuanzisha Programu ya Mafunzo katika Halmashauri zote Nchini kupitia OR-TAMISEMI kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali zenye majukumu yanayoendana na kuwajengea uwezo wajasiriamali kama vile TRA, TBS, TRDO, SIDO, TANTRADE na TCCIA ambazo zote zina majukumu ya kuhakikisha elimu ya viwango, utambuzi wa bidhaa na masoko kuwa zinawafikia wananchi wote kwa kuanzia ngazi ya Halmashauri".
Dkt. Gwajima ameongeza kuwa, awali ukosefu wa huduma ya msimbomilia nchini ulifanya bidhaa kutotambulika katika mifumo ya kimataifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wakati wa mauzo hivyo Serikali kukosa mapato kupitia ongezeko la thamani kwenye bidhaa zinazouzwa kwa njia ya reja reja.
Waziri Dkt. Gwajima amebainisha kwamba Tanzania ni kati ya nchi chache Afrika kupata leseni ya Shirika la GS1 Global lenye hati miliki ya huduma ya msimbomilia ambapo nchi nyingine ni Algeria, Misri, Ivory Coast, Kenya, Libya, Mauritius, Morocco, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini hali inayochangia Tanzania kutoa huduma hiyo kwa nchi zinazoizunguka na kupanua wigo wa wateja.
Ametoa wito kwa Uongozi na Menejimenti ya GS1 Tanzania kuwa na mikakati ya kuzifikia nchi jirani kuhakikisha wanatumia Msimbomilia (Barcodes) za Tanzania ili kuongeza pato na kuitangaza nchi.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa GS1 Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Majukwaa ya Uwezeseshaji Wanawake Kiuchumi, Fatma Kange amebainisha changamoto ya wafanyabiashara wengi kukosa maeneo ya uzalishaji wa bidhaa zao na kuiomba Serikali kuona namna ya kuwapa maeneo.
"Wazalishaji wengi bado wanafanyia shughuli zao nyumbani, hivyo tunaomba tukipata eneo la ekari 10 tu popote hapa Dar es salaam".
No comments:
Post a Comment