A: UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania
(TPA) ilianzishwa kupitia Sheria Na. 17 ya mwaka 2004. Mamlaka hii
ilirithi na kuchukua majukumu ya iliyokuwa Mamlaka ya Bandari
Tanzania (Tanzania Harbors Authority-THA) iliyoanzishwa kupitia
Sheria ya Mamlaka ya Bandari Na. 12 ya mwaka 1977 baada ya
kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kupewa
majukumu zaidi ya kumiliki, kuendesha na kuendeleza bandari zilizopo
pwani ya Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu.
2. Mheshimiwa Spika, Sheria hiyo ya Bandari Na. 17 ya Mwaka 2004
inaipa TPA majukumu ya kumiliki, kusimamia, kuendesha na
kuendeleza maeneo yote ya bandari Tanzania Bara. Madhumuni
makuu ya kuanzishwa kwa TPA yameainishwa katika Kifungu cha (5)
cha Sheria hiyo ambayo ni kuhakikisha Tanzania inaendelea
kunufaika na faida ya kijiografia ikiwemo: kuchagiza usimamizi bora na
ufungamanishaji wa tija wa bandari zilizopo pwani ya Bahari ya Hindi
na Maziwa Makuu; kuhakikisha kunakuwa na tija katika huduma
zinazotolewa za upakiaji na ushushaji wa mizigo pamoja na abiria;
kuendeleza, kuboresha na kusimamia miundombinu ya kibandari;
kusimamia usalama wa bandari; na kuingia mikataba au makubaliano
na mtu au taasisi yoyote kwa ajili ya utoaji wa huduma za bandari.
3. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwekeza kwenye bandari
zake kwa vipindi tofauti kwa kutumia vyanzo vyake na fedha za mikopo katika kutekeleza mikakati kwa lengo la kuboresha sekta ya
bandari nchini. Mkakati uliochukuliwa hivi karibuni ni utekelezaji wa
Mradi mkubwa wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam (Dar es
Salaam Maritime Gateway Project – DMGP) ambao umehusisha:
uimarishaji na uongezaji wa kina cha Gati Na. 1-7; ujenzi wa gati
jipya la kuhudumia magari; na uongezaji wa kina cha lango la kuingia
bandarini. Uzoefu umeonesha kuwa uwekezaji wa namna hii una faida
kubwa kwa nchi iwapo bandari itaendeshwa kwa tija na ufanisi
mkubwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
4. Mheshimiwa Spika, pamoja na kuchukua hatua mbalimbali za
maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam, bado ufanisi katika utoaji
huduma za bandari haujafikia viwango vinavyotakiwa kimataifa. Hali
ya sasa ya utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuwa
ya kiwango cha chini ikilinganishwa na bandari shindani kikanda. Kwa
mfano, wastani wa meli kusubiri nangani kwa Bandari ya Dar es
salaam ni siku 5 ikilinganishwa na siku 1.25 kwa Bandari ya Mombasa
na siku 1.6 kwa Bandari ya Durban. Ufanisi mdogo wa Bandari ya Dar
es Salaam umetokana na changamoto mbalimbali zikiwemo:
kukosekana kwa mifumo ya kisasa ya TEHAMA; kutokuwepo kwa
maeneo ya kutosha ndani na nje ya bandari kwa ajili ya kuhifadhia
shehena pamoja na maegesho ya meli; na kukosekana kwa mitambo
ya kutosha na ya kisasa ya kuhudumia shehena ambayo teknolojia
yake inabadilika mara kwa mara na ina gharama kubwa ya uwekezaji
na uendeshaji.
5. Mheshimiwa Spika, athari za kutokuwa na ufanisi katika Bandari ya
Dar es Salaam ni pamoja na: meli kusubiri muda mrefu nangani
ambako kunasababisha kuongezeka kwa gharama ya kutumia bandari
ya Dar es Salaam, kwa mfano gharama za meli kusubiri nangani kwa
siku moja ni takriban Dola za Marekani 25,000, sawa na takriban
Shilingi milioni 58 kwa siku; meli kutumia muda mrefu kupakia na
kupakua shehena gatini kwa wastani wa siku 5 ikilinganishwa na siku
1 inayokubalika kimataifa; meli kubwa kutokuja katika bandari ya Dar
es Salaam kutokana na kuchukua muda mrefu kuhudumiwa. Hali hii
husababisha bandari yetu kuwa bandari inayolishwa shehena na
bandari zingine (feeded port) na hivyo kuongeza gharama ya kutumia
bandari hiyo na kuikosesha nchi mapato ambayo yangeweza kutumika
katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini ambayo
ingesaidia kukuza uchumi na kuboresha huduma za wananchi. Pia,
kunaongeza gharama katika mnyororo mzima wa usafirishaji (total
route costs) kutoka nje ya nchi, kupitia katika bandari yetu kwenda
nchi za jirani zinazotumia bandari hiyo. Kwa mfano, gharama ya
kusafirisha kasha moja kutoka nje ya nchi (on transit) kwenda nchi ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zinafikia takriban Dola za
Marekani kati ya 8,500 hadi 12,000. Hii ni gharama kubwa sana
ikilinganishwa na Bandari shindani.
6. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua kuwa Serikali pekee haitaweza
kutatua changamoto zilizopo kwenye Bandari ya Dar es salaam,
kuanzia miaka ya 2000, Serikali ya Awamu ya Tatu kupitia Tume ya
Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) iliingia mkataba wa
upangaji na uendeshaji (lease and concession agreement) na
Kampuni ya Kimataifa ya Uendeshaji wa Vitengo vya Makasha,
Hutchison ya Hong-Kong China. Mkataba huo ulidumu kwa miaka
ishirini na mbili (22) kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2022 na uliipa
haki ya kipekee Kampuni hiyo kwa ajili ya kuendesha shughuli za
kuhudumia makasha katika gati namba 8 hadi 11 za Bandari ya Dar es
Salaam. Wakati huo huo TPA ikiendesha na kuhudumia maeneo
mengine ya Bandari hiyo.
Mheshimiwa Spika, ili kutatua changamoto za Bandari zilizopo na
kwa kuzingatia dhima ya Serikali ya kuboresha Sekta ya Bandari
nchini ili kuongeza ufanisi na mchango wa Sekta ya Bandari katika
mapato ya nchi, ajira na kuchagiza sekta nyingine za kiuchumi,
Serikali ilifanya maamuzi ya kutafuta Wawekezaji wapya wanao
endana na dhima ya Serikali. Hatua hizo zilihusisha kupokea
mapendekezo ya Wawekezaji mbalimbali wakiwemo kampuni ya
Hutchson (Hong Kong), Antewerp/Brugge (Belgium), PSA International
(Singapore), DP World (Dubai), Abu Dhabi Ports (Abu Dhabi), Adani
Ports and Logistics (Mundra-India), Kampuni ya CMA-CGM (France)
pamoja na Kampuni ya Maersk (Denmark). Lengo kuu ni kufungua
masoko ya kimkakati katika eneo la bidhaa na biashara ya usafirishaji
ndani ya nchi na kanda zinazotuzunguka.
8. Mheshimiwa Spika, katika kupitia mawasilisho ya kampuni hizo
pamoja na sifa zao kimataifa, Serikali iliamua kuanzisha majadiliano
na kampuni ya DP World kwa kuzingatia uzoefu wake katika
uendeshaji wa shughuli za bandari barani Afrika, Asia, Ulaya na
Amerika ya Kaskazini na Kusini. Kampuni hii ina uzoefu na utaalamu
wa kuchagiza mnyororo mzima wa usafirishaji (end to end total
logistics chain solution) kutoka maeneo ambayo bidhaa zinatoka
mpaka kufika kwa Walaji. Uendeshaji wa maeneo maalum ya kiuchumi
(special economic zones) karibu na bandari, usafirishaji baharini na
nchi kavu (kupitia njia ya reli), uwekezaji mkubwa katika maeneo
mbalimbali ambayo imewekeza na pamoja kuajiri Wazawa katika
maeneo hayo. Aidha, kwa upande wa makampuni mengine ambayo
TPA ilipokea mapendekezo yao, yalionesha nia ya kuwekeza
bandarini pekee na sio kuchagiza mnyororo mzima wa usafirishaji.
Pia, baadhi ya makampuni hayo hayana uzoefu wa kuendesha
shughuli za bandari barani Afrika wakati Kampuni ya DP World
inaendesha takriban bandari sita (6) barani Afrika na bandari zaidi ya
30 duniani kote kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia nia ya Serikali kuvutia uwekezaji
nchini, wakati wa maonesho ya Dubai Expo 2020 tarehe 28 Februari,
2022 Hati za Makubaliano takriban 30 zilisainiwa baina ya Taasisi za
Serikali ya Tanzania na Sekta binafsi na Taasisi za Serikali za Dubai
kwa lengo la kuvutia uwekezaji nchini ili kuchochea ukuaji wa uchumi
na maendeleo ya nchi. Moja kati ya Hati ya Makubaliano hayo ni
baina ya TPA na DP World iliyolenga kuanzisha ushirikiano wa
uboreshaji, uendeshaji na uendelezaji wa maeneo ya bandari nchini.
10. Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha utekelezaji wa Hati ya Makubaliano
hayo, Serikali iliteua Timu ya Wataalam ambayo ilipewa jukumu la
kufanya majadiliano na Wataalam wa Serikali ya Dubai na kufanikisha
kuandaliwa na kusainiwa kwa Mkataba baina ya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa mujibu wa taratibu
zilizopo. Mkataba huo ni kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii
kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari
Tanzania.
11. Mheshimiwa Spika, lengo la Mkataba huu ni kuweka msingi wa
makubaliano (framework agreement) baina ya nchi na nchi ili
kuwezesha kuanza kufanyika kwa majadiliano na kuingiwa kwa
mikataba mbalimbali (Mikataba ya Nchi Mwenyeji, Upangishaji na
Uendeshaji) ya uwekezaji na uendeshaji wa maeneo ya bandari
nchini.
12. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa masharti ya Mkataba huo
unapaswa kuridhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa mujibu wa Ibara ya 63(3)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ya mwaka 1977 ili utekelezaji wake uweze kuanza.
Hivyo, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ilianzisha
mchakato wa kupata ridhaa ya Serikali ya kuwasilisha Mkataba huu Bungeni kwa ajili ya kuridhiwa.
B: UFAFANUZI KUHUSU MKATABA WA IGA
13. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Ibara ya 2 ya Mkataba wa IGA,
lengo lake ni kuweka msingi wa ushirikiano baina ya Serikali mbili kwa
maeneo mahsusi yaliyoainishwa ndani ya Mkataba husika (Rejea
Appendix 1 ya Mkataba) ambayo utekelezaji wake utafanyika kupitia
Mikataba Mahsusi baina ya taasisi zilizoainishwa katika Mkataba wa
IGA kama taasisi tekelezi ambazo ni TPA na DP World. Hivyo,
Mkataba huu hauna masharti yanayoifunga Serikali kuhusu maeneo
ya ushirikiano yaliyoanishwa pasipo uwepo wa Mikataba Mahsusi wa
utekelezaji wa miradi itayojadiliwa na kukubaliwa na pande mbili.
14. Mheshimiwa Spika, Mawanda ya uwekezaji chini ya Mkataba huu
yatahusisha uendelezaji na uendeshaji wa baadhi ya maeneo ya
Bandari na sio bandari yote kwa ujumla wake. Aidha, uendelezaji na uendeshaji huo utafanyika kupitia Mikataba Mahsusi ya Miradi (Project
Agreements) ambayo itajadiliwa na kuingiwa kwa kila eneo la
ushirikiano na itahusisha matumizi ya ardhi pekee na sio umiliki wa
ardhi ikiwa ni pamoja na Serikali kuhakikisha kuwa Sheria, kanuni na
taratibu za nchi zinazolinda umiliki ya ardhi ya Watanzania
zinazingatiwa na kusimamiwa ipasavyo.
15. Mheshimiwa Spika, Mkataba huu umeainisha Awamu kuu mbili za
maeneo ya ushirikiano. Awamu ya kwanza itajumuisha: kusimamia,
kuendesha na kuendeleza baadhi ya Magati katika Bandari ya Dar es
Salaam; kuboresha Gati la Majahazi na Gati la Abiria katika Bandari
ya Dar es Salaam ili kuvutia vyombo vikubwa zaidi na meli za kitalii
kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam; kuwekeza katika
maeneo yaliyotengwa katika Bandari Kavu; kufanya uwekezaji katika
Mifumo ya Kisasa ya TEHAMA ya kuendeshea shughuli za kibandari ili
kuongeza ufanisi wa Bandari kuwa shindani; na kuwajengea uwezo
Watumishi wa TPA ili waweze kutekeleza shughuli za Bandari kwa
ufanisi katika maeneo mengine ya Bandari Nchini. Msisitizo wa
Serikali ni kuhakikisha maeneo yote ya nchi yanabaki chini ya umiliki
wa Serikali.
16. Mheshimiwa Spika, Katika Awamu ya Pili ya Miradi (Phase II),
majadiliano yatafanyika kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo:
kuongeza thamani ya bidhaa; maeneo ya viwanda na miundombinu
mingine itakayoongeza ufanisi katika usafirishaji wa bidhaa kwenda na
kutoka nchi zinazotuzunguka; kuwekeza katika Bandari zingine za
Bahari na Maziwa kama itavyopendekezwa na Serikali kupitia TPA
kwa kuzingatia ulinzi na maslahi mapana ya Taifa; na kuwekeza katika
vyombo vya usafirishaji wa shehena (matishari) katika maziwa makuu
ili kuunganisha bandari za Maziwa Makuu na bandari za nchi jirani
kama itakavyopendekezwa na TPA na kukubaliana na Mwekezaji.
17. Mheshimiwa Spika, Ili kutoa fursa kwa Wawekezaji wengine
kuwekeza katika maeneo mengine ya bandari nchini kwa lengo la
kuleta ushindani, tija na ufanisi, uwekezaji tarajiwa chini ya Mkataba
huu hautahusisha maeneo ya Gati namba 8 hadi 11 (Kitengo Na. 2
cha Makasha), Gati la Mafuta Kurasini Na. 1 (KOJ 1), Gati la Mafuta
Kurasini Na. 2 (KOJ2), Boya la Kupokelea Mafuta (SBM) na Gati la
Kuhudumia Magari katika Bandari ya Dar es Salaam pamoja na
maeneo yote ya Awamu ya Kwanza na Pili ambayo hayatafikia
muafaka katika majadiliano yatakayofanyika baada ya kuridhiwa kwa
IGA. Uwekezaji huo pia, hautahusisha Bandari ya Tanga na Mtwara.
18. Mheshimiwa Spika, Mkataba huu unatoa haki ya upekee ya kufanya
majadiliano kwa Awamu ya Miradi iliyoanishwa kwenye Mkataba huo
kwa kipindi kisichozidi miezi kumi na mbili (12). Msingi wa kutoa haki
hii ya kipekee ni kuwezesha pande mbili kufanya majadiliano na
kumpa uhakika Mwekezaji kujadiliana katika maeneo pasipo kuwepo
kwa majadiliano na Mwekezaji mwingine katika maeneo hayo hayo.
Hivyo, iwapo kipindi hicho kitakwisha bila kufikia makubaliano, TPA
inaweza kuanzisha majadiliano na Wawekezaji wengine katika
maeneo hayo pasipo kuwepo kwa mgogoro wowote chini ya Mkataba
huo.
19. Mheshimiwa Spika, Kuhusu muda, Mkataba huu utakuwa hai mpaka
pale ambapo shughuli za miradi zitasitishwa au kuisha kwa muda wa
mikataba ya nchi mwenyeji na mikataba ya miradi. Msingi wa Mkataba
huu kuendana na mikataba ya miradi ni kutokana na kwamba
unaweka msingi unaowezesha kuingia na kutekelezwa kwa mikataba
hiyo nchini. Iwapo Mkataba huu utakuwa na ukomo kabla ya kuisha
mikataba ya miradi iliyo chini ya Mkataba huu, utekelezaji wa mikataba
ya miradi baada ya kuisha kwa mkataba huu itakuwa batili. Vile vile,
uhai wa Mkataba huu utawezesha kuingiwa kwa mikataba mbalimbali
yenye masharti na muda wa ukomo tofauti na ambayo yote
inategemea msingi wa uhai wa mkataba huu. Hivyo, endapo upande
mmoja wa mkataba huu utajitoa, athari yake ni kufa au kuvunjika kwa
utekelezaji wa mikataba yote ya miradi iliyoanzishwa chini ya Mkataba
huu.
20. Mheshimiwa Spika, jukumu la Ulinzi na Usalama katika Bandari ya
Dar es Salaam litaendela kusimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia vyombo vyake vya Ulinzi na Usalama
ambavyo vipo katika maeneo yote ya Bandari kwa kuzingatia Sheria
za nchi na mikataba ya kimataifa. Suala hili limezingatiwa pia katika
Mkataba wa IGA na kuwekwa bayana kwamba masuala ya Ulinzi na
Usalama hayatakiukwa kwa namna yeyote wakati wa utekelezaji
shughuli za uwekezaji. Vilevile, taasisi zote za Serikali ambazo
zinahusika katika shughuli za bandarin zitaendelea kutekeleza
majukumu yao kwa mujibu Sheria ndani ya eneo la bandari. Uwepo
wa sekta binafsi kutoa huduma katika maeneo ya bandari umeendelea
kuwepo na kusimamiwa na Serikali kwa miongo tofauti tofauti. Aidha,
katika kipindi chote ambacho Sekta Binafsi imehusishwa katika
uendeshaji wa bandari, hakujawahi kujitokeza tukio la kuhatarisha
usalama wa nchi.
21. Mheshimiwa Spika, naomba kuwataarifu kwamba, uwepo wa ajira za
Watanzania hususan watumishi wa bandari ya Dar es Salaam ni
kipaumbele kikubwa cha Serikali sio tu katika Azimio hili bali katika kila
aina ya uwekezaji ambao nchi itaufanya. Ibara ya 13 ya Mkataba huu
inaitaka DP World kuendeleza ajira za Watumishi wote waliopo,
kuwaajiri Watanzania pamoja kuwaendeleza kitaaluma. Vilevile,
Mkataba huu umeweka bayana sharti kwa Kampuni ya DP World
kutumia Wakandarasi wa ndani katika manunuzi ya huduma na bidhaa
pamoja na kusaidia Vyuo vya mafunzo vya Tanzania katika masuala
ya elimu ya usafirishaji majini.
22. Mheshimiwa Spika, naomba pia kuchukua fursa hii kuelezea
manufaa ambayo yanatarajiwa kupatikana iwapo Bunge letu Tukufu
litaridhia Azimio hili na kuwezesha Serikali kuendelea na hatua
zinazofuata za majadiliano na Serikali ya Dubai. Baadhi ya manufaa
yatakayopatikana ni pamoja na:
i. Kupunguza muda wa meli kukaa nangani kutoka siku 5 kwa
sasa mpaka masaa 24. Hii itapunguza gharama za utumiaji
wa Bandari yetu. Matokeo yake itaongeza idadi ya meli
zitazokuja Bandari ya Dar es Salaam kutoka meli 1,569
zilizohudumiwa mwaka 2021/22 mpaka kufikia takriban meli
2,950 ifikapo mwaka 2032/33;
ii. Kupunguza muda wa ushushaji wa makontena kutoka siku 4.5
mpaka siku 2;
iii. Kupunguza muda wa uondoshaji mizigo kutoka masaa 12
mpaka saa 1 kutokana na uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA;
iv. Kupunguza gharama ya usafirishaji wa mizigo kutoka nchi za
nje kwenda nchi za Jirani, kwa mfano kutoka US$ 12,000
mpaka kati ya US$6,000 na US$7,000 kwa kasha
linalokwenda nchi ya Malawi, Zambia au DRC. Hii italeta
Watumiaji wengi kwenye Bandari ya Dar es Salaam;
v. Kuongezeka kwa shehena inayohudumiwa kutoka tani milioni
18.41 za mwaka 2021/22 hadi kufikia tani milioni 47.57 mwaka
2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 158;
vi. Kuongezeka kwa Mapato ya Serikali yatokanayo na Kodi ya
Forodha inayokusanywa katika shehena inayopitishwa
bandarini kutoka Shilingi Trilioni 7.76 za mwaka 2021/22 hadi
Shilingi Trilioni 26.7 za mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la
asilimia 244;
vii. Kuongezeka kwa ajira zinazotokana na shughuli za bandari
kutoka 28,990 mwaka 2021/22 hadi ajira 71,907 ifikapo
mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 148;
viii. Maboresho ya maeneo ya kuhudumia shehena ya makasha
na kuweka mitambo yenye Teknolojia ya kisasa;
ix. Kuendeleza eneo la kuhifadhia mizigo la Bandari Kavu kwa
kuweka miundombinu ya kisasa ya kuhudumia aina zote za
shehena;
x. Maboresho ya magati ya kuhudumia Majahazi na Abiria ikiwa
ni pamoja na kushawishi uingiaji wa meli kubwa za kitalii
zitakazo ongeza idadi ya Watalii nchini na kuongeza pato la
Taifa;
xi. Kusimika Mifumo ya TEHAMA kwa ajili ya shughuli za bandari
na kuwaunganisha wadau wake;
xii. Mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa TPA katika
Bandari zote (knowledge and skills transfer);
xiii. Uanzishwaji wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi/Viwanda; na
xiv. Kuchochea ukuaji wa sekta zingine za kiuchumi zikiwemo
Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi; kuchagiza shughuli za
Viwanda na Biashara; kuchagiza ukuaji wa sekta ndogo za
usafirishaji kwa njia ya reli (SGR, TAZARA na MGR) na
barabara; Watanzania kunufaika na teknolojia na ujuzi wa
uendeshaji wa bandari kisasa; na kujenga mahusiano ya
kidiplomasia.
23. Mheshimiwa Spika, iwapo Bunge lako litaridhia Mkataba huu, Serikali
itahakikisha wakati wa kuandaa Mikataba ya Utekelezaji wa miradi
iliyo chini ya Mkataba huu masuala muhimu yafuatayo yatazingatiwa:
i. Mikataba itakayoandaliwa itaweka bayana kipindi cha
utekelezaji wake na ukomo, muda wa marejeo na viasharia
muhimu vya ufanisi wa kiutendaji (key performance
indicators);
ii. Uandaaji wa mikataba ya miradi utafanywa chini ya usimamizi
wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuzingatia
maslahi mapana ya Taifa;
iii. Mikataba itakayoandaliwa italinda ajira za Wafanyakazi
Wazawa na kuwajengea uwezo;
iv. Mifumo yote ya TEHAMA itakayosimikwa na DP World
inasomana na Mifumo ya Serikali;
v. Taasisi mahsusi za Serikali zitaendelea na utekelezaji wa
majukumu yake katika maeneo yote ya bandari; na
vi. Kuhakikisha DP World anachukua hatua stahiki za masuala ya
utafutaji wa masoko ya Bandari ya Dar es Salaam.
24. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya ya awali naomba sasa
niwasilishe Azimio la kuridhia Kuridhia Mkataba baina ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu
Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii ya Uendelezaji na Uboreshaji wa
Utendaji Kazi wa Bandari Tanzania.
No comments:
Post a Comment