Matumizi ya Vyama vya Ushirika kusambaza mbolea kwamkosha Katibu Tawala Geita, Prof. Kanyarara - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, June 6, 2023

Matumizi ya Vyama vya Ushirika kusambaza mbolea kwamkosha Katibu Tawala Geita, Prof. Kanyarara

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Prof. Godius W. Kanyarara akizungumza jambo na timu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) (hawapo pichani) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ruzuku, Louis Kasera tarehe 05 Juni, 2023.
Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Ziwa, Dkt. Asheri Kalala akizungumza jambo wakati wa kikao baina ya TFRA na Wakuu wa Idara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Mkoa na wilaya za Geita (hawapo pichani) tarehe 05 Juni, 2023
Wakuu wa Idara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Mkoa wa Geita, Mrajisi na viongozi wa vyama vya ushirika wa mkoani humo wakifuatilia mada katika kikao baina yao na wataalamu kutoka TFRA waliofika kujadili na kupendekeza namna bora ya kufikisha mbolea kwa wakulima kilichofanyika tarehe 05 Juni, 2023 katika ukumbi wa Mkoa wa Geita
Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Geita, Dkt. Elfas Mseya akitoa neno la shukrani kwa TFRA na kuahirisha kikao mara baada ya kikao cha kuwajengea uwezo na kujadili namna bora ya kuwafikishia mbolea wakulima msimu wa kilimo 2023/2024 kufikia mwisho na kuwataka wajumbe kwenda kutekeleza kwa mujibu wa makubaliano waliyofikia.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Prof. Godius W. Kanyarara (mwenye suti) akimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Ruzuku, Louis Kasera (mwenye t-shirt ya kijani) alipokuwa akizungumza katika kikao kifupi kilichofanyika ofisini kwake tarehe 05 Juni, 2023
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Prof. Godius W. Kanyarara akizungumza jambo wakati wa kikao kifupi ofisini kwake baina ya wataalamu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ruzuku, Louis Kasera (mwenye tshirt ya kijani) walipofika kueleza nia ya kufika mkoani hapo ikiwa ni pamoja na kuhamasisha usajili wa wakulima pamoja na kuvishirikisha vyama vya ushirika katika zoezi la kusambaza mbolea za ruzuku kwa wakulima


Na Mwandishi wetu Geita

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Prof. Godius W. Kanyarara amepongeza uamuzi wa Serikali wa kutumia vyama vya ushirika katika kusambaza mbolea kwa msimu wa kilimo 2023/2024.


Amesema, Vyama vya ushirika viko kwa wananchi na vinajua changamoto za wakulima na namna ya kuzitatua hivyo vitasaidia sana kupunguza malalamiko ya wakulima.


Katibu Tawala Prof. Kanyarara alitoa kauli hiyo tarehe 5 Juni, 2023 ofisini kwake akiwa katika kikao kifupi baina yake na timu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ruzuku Louis Kasera.


Aidha, Prof. Kanyarara aliiomba TFRA kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya mbolea vya ndani ili kupunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi na kueleza uzalishaji wa ndani utaongeza ufanisi zaidi katika kukuza kilimo na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni katika kuagiza mbolea nje ya nchi na baadaye kukuza uchumi wa nchi.


"Lazima tujitosheleze kwa chakula, mbolea, viuwatilifu, utafiti na gesi ili kuongeza mchango wa Sekta ya Kilimo kwenye mfuko wa taifa", Kanyarara alikazia.


Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ruzuku, Louis Kasera alieleza lengo la kufika mkoani hapo kuwa ni pamoja na kuhamasisha watendaji kuendelea na zoezi la usajili na uhuishaji wa taarifa za wakulima ili kuwawezesha kunufaika na mbolea za ruzuku kwa msimu wa kilimo 2023/2024.


Alisema, serikali imejipanga kutumia Vyama vya Ushirika kufikisha mbolea kwa wakulima na kubainisha kuwa, Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) itasaidia kufikisha mbolea kwenye maeneo yasiyofikika na hivyo kuwawezesha wakulima kutokwenda zaidi ya Kilomita 15 kufuata pembejeo ya mbolea.


Aidha, Kasera alieleza kuwa, ifikapo tarehe mosi Julai mbolea zitakuwa zimefikishwa karibu na wakulima na kutoa wito kwa wakulima kujitokeza kununua mbolea na kupunguza misururu mirefu  wakati wa msimu.


"Nguvu kubwa tunataka kuweka kwenye vyama vya ushirika na kueleza Chama Kikuu cha Ushirika cha Tarime (WAMAKU) kilisaidia sana katika kusambaza mbolea msimu uliopita katika maeneo ya Tarime na Serengeti na hivyo serikali  ikaona ni vyema kutumia vyama hivyo ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wakulima.


Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Geita, Dkt. Elfas Mseya aliishukuru  TFRA kwa kuanza mchakato wa maandalizi ya msimu wa kilimo mapema na kueleza hii itasaidia kupunguza changamoto za misururu mirefu ya kununua mbolea kwa mawakala.


Aidha, ameipongeza TFRA kwa kukutana na watendaji katika kata za mikoa na wilaya kwani itawapa wepesi katika kusimamia mchakato mzima wa kusajili, kuhuisha na kusimamia usambazaji wa mbolea kwa wakulima.

No comments:

Post a Comment