MHE. SIMBACHAWENE AWATAKA WAHITIMU WA TPSC KUFAHAMU KUWA UTUMISHI WA UMMA NI IBADA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, June 3, 2023

MHE. SIMBACHAWENE AWATAKA WAHITIMU WA TPSC KUFAHAMU KUWA UTUMISHI WA UMMA NI IBADA


Na. Veronica Mwafisi-Tanga


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewataka wahitimu wa kozi mbalimbali katika mahafali ya 37 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kufahamu kuwa utumishi wa umma ni ibada, hivyo watakapopata fursa ya kuajiriwa katika taasisi za umma itawapasa kufanya kazi kwa kuzingatia uadilifu na kujitoa katika kuwahudumia wananchi ili kutimiza ibada hiyo kwa maendeleo ya taifa.
Mhe. Simbachawene ametoa nasaha hizo kabla ya kuwatunuku wahitimu wa kozi mbalimbali katika mahafali ya 37 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika Mkoani Tanga.


Mhe. Simbachawene amesema, utumishi wa umma umelenga katika kuwahudumia wananchi na sio sehemu ya kutengeneza faida, hivyo wahitimu hao watakapopata fursa ya kuajiriwa serikalini ni lazima wazingatie hilo.



“Kuna tofauti sana kati ya mtumishi anayeajiriwa katika utumishi wa umma na mtumishi anayetumikia sekta binafsi, utumishi wa umma ni ibada na kujitoa, kwenye utumishi wa umma tunahudumia wananchi lakini kwenye sekta binafsi wao wanatengeneza faida, utumishi wa umma unahitaji unyenyekevu katika kuwahudumia wananchi na sio sehemu ya kujitafutia masilahi binafsi,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.


Ili kuwa na watumishi walio na maadili, Mhe. Simbachawene ameusisitiza uongozi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kutilia mkazo katika kusimamia na kufundisha maadili jambo ambalo litasaidia pia kuwatengeneza watumishi wenye uvumilivu watakaoweza kufanya kazi na kuwahudumia wananchi sehemu yoyote watakayopangiwa bila kuwa na manungúniko.


Kutokana na changamoto nyingi za kiutumishi zilizopo, Mhe. Simbachawene ameulekeza uongozi huo wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, kufanya tafiti za masuala mbalimbali ya kiutumishi ambazo zitawawezesha Viongozi wa Nchi kufanya maamuzi sahihi yanayohusiana na maendeleo ya utumishi wa umma.


Mhe. Simbachawene amesema Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, ndicho chenye jukumu la kufanya utafiti wa masuala mbalimbali ya kiutumishi, hivyo wanatakiwa kuwekeza kwenye kufanya utafiti na kuandika taarifa zitakazotumiwa na viongozi kufanya maamuzi ya kisera na kisheria ili kuboresha utumishi wa umma kwani huwezi kufanya maamuzi bila kufanya tafiti.



Katika kuhakikisha wanachuo wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Kampasi ya Tanga, wanapata elimu katika mazingira mazuri kama ilivyo katika Kampasi nyingine za chuo hicho, Mhe. Simbachawene amewaelekeza Watendaji wa Ofisi yake kwa kushrikiana na Uongozi wa Mkoa wa Tanga kutafuta eneo zuri ambalo wanachuo watapata nafasi ya kujifunzia tofauti na la sasa ambalo majengo yake hayaridhishi.


Aidha, Mhe. Simbachawene ameupongeza Uongozi wa Mkoa wa Tanga na wananchi wa mkoa huo kwa kuona umuhimu wa elimu na kuamua kutoa eneo la Maweni ambalo Kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania itajengwa.


Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mjini, Mhe. Hashim Mgandilwa ameipongeza Serikali kwa uamuzi wake mzuri wa kuanzisha Kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania jijini Tanga kwani itasaidia kuleta chachu kwa wazazi na familia ambazo zinaishi ukanda wa Pwani kupata mwamko wa elimu.



Kwa Upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejiementi ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amewasihi wahitimu kuzingatia uadilifu na utendaji mzuri watakapopata fursa ya kuajiriwa katika utumishi wa umma na hata katika sekta binafsi kwani uadilifu unahitajika katika maeneo yote kwa manufaa ya nchi


Bw. Mkomi amesema yeye akiwa ndiye Mtendaji wa Ofisi ya Rais -UTUMISHI atazifanyia kazi changamoto zote za Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania ikiwemo ya kukamilisha utaratibu wa upatikanaji wa hati eneo la Maweni lililotolewa na Mkoa wa Tanga na wananchi ili kuanza kwa ujenzi wa Kampasi ya Tanga na kutafuta eneo ambalo wanachuo watapata fursa ya kujisomea katika hali yenye ubora. 


Akiwasilisha taarifa kuhusu mahafali ya 37 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Kaimu Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Dkt. Ernest Mabonesho amesema jumla ya wahitimu 1,803 kutoka katika kampasi zote sita za TPSC ambazo ni Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Tabora, Singida na Mbeya wametunukiwa vyeti katika ngazi ya shahada, stashahada na astashahada katika kozi mbalimbali.

No comments:

Post a Comment