MITAWI: TUMECHUKUA HATUA NA MIKAKATI MADHUBUTI BIASHARA YA KABONI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, June 19, 2023

MITAWI: TUMECHUKUA HATUA NA MIKAKATI MADHUBUTI BIASHARA YA KABONI


Serikali imesema imeandaa hatua na mikakati madhubuti yenye kuibua fursa za miradi ya kijamii kwa wananchi ikiwemo kanuni na mwongozo wa biashara ya kaboni ikiwa ni njia mbadala ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.


Hayo yameelezwa leo Jumatatu (Juni 19, 2023) na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Abdallah Hassan Mitawi wakati akifunga warsha ya siku moja baina ya wahariri wa vyombo vya habari na Menejimenti ya Ofisi hiyo iliyolenga kujenga uelewa kuhusu kanuni na mwongozo wa biashara ya kaboni.


Mitawi amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoathiriwa na athatri za mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa isiyotabirika hali inayojidhihirisha kupitia matukio ya mvua zisizotabirika, ongezeko la joto, ukame na mafuriko, ambapo athari hizo zimeathiri sekta za kijamii na kiuchumi.


“Pamoja na changamoto zinazochangiwa na mabadiliko ya tabia nchi kumekuwa na fursa na jitihada mbalimbali ambazo zimechukuliwa na serikali ikiwa ni pamoja na mapitio ya sera, uandaaji wa kanuni, mikakati na miongozo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi” amesema Mitawi.


Akifafanua zaidi Mitawi amesema biashara ya kaboni ni mojawapo ya nyenzo muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani inayotekelezwa na nchi wanachama wa Maktaba wa Mabadiliko ya tabianchi, itifaki ya Kyoto na makubaliano ya Paris, ambapo Tanzania ni mwanachama wa mikataba hiyo.


Kwa mujibu wa Mitawi pamoja na kuwepo kwa sera na mikakati mbalimbali, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa Kanuni na mwongozo wa usimamizi wa biashara ya kaboni ya mwaka 2022 ili kuweka utaratibu na masharti yanayopaswa kuzingatiwa na wadau na wawekezaji wa biashara hiyo nchini.


“Kanuni na mwongozo wa biashara ya kaboni tayari zilishatangazwa kupitia Gazeti la Serikali Na. 636 la tarehe 28 Oktoba, 2022 na hivyo kuwa tayari kwa matumizi. Nyenzo hizi zimejikita katika kuimarisha mchango wa nchi katika jitihada za kupunguza uzalishaji wa gesi joto” amesema Mitawi.


Akiwasilisha mada kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Andrew Komba amesema Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani imeendelea kushuhudia uharibifu wa mazingira ikiwemo uchafuzi wa bahari, mito na vyanzo vya maji, ukataji wa miti na upotevu wa bionuai, kuongezeka kwa joto la dunia, mabadiliko ya tabianchi.


Dkt. Komba amesema katika kukabiliana na athari hizo, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kutumia mbinu mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi ikiwemo kupunguza uzalishaji wa gesijoto na kuzijengea uwezo jamii kustahimili athari za mabadiliko ya tabia nchi kupitia mbinu mbalimbali ikiwemo kilimo cha umwagiliaji, uchimbaji wa mabwawa na kujenga miundombinu ya kudhibiti mafuriko na mmomonyoko wa udongo


Akiwasilisha mada kuhusu Mchakato wa Usimamizi wa Biashara ya Kaboni, Mkurugenzi wa Kituo cha Kitaifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) Prof. 
Eliakimu Zahabu amesema Mwaka 1997 Umoja wa Mataifa ulianzisha Itifaki ya Kyoto ambayo ilizitaka nchi zilizoendelea kupunguza uzalishaji wa gesijoto kwa 5%.


Prof. Zahabu amesema kwa kuzingatia umuhimu wa biashara hiyo, itifaki hiyo iliweka usimamizi wa biashara ya Kaboni katika ngazi mbili ambayo ni Ngazi ya kimataifa unayohusisha uaandaaji wa huandaa sera na miongozo, mfumo au utaratibu wa kimataifa pamoja na ngazi ya kitaifa inayohusisha Mwongozo na Kanuni za biashara ya kaboni.


Aidha Prof. Zahabu amesema Kituo hicho imeendelea kuchukua hatua na mikakati endelevu ya kujenga uelewa kwa jamii kuhusu biashara ya kaboni katika ngazi zote ili kuvutia wawekezaji na wadau na kuhakikisha kuwa Tanzania ina inanufaika na biashara ya kaboni kiuchumi sambamba na utunzaji wa mazingira.

No comments:

Post a Comment