Na Mwandishi wetu Tabora
Imeelezwa kuwa, Mkoa wa Tabora umetuma takribani tani 8,000 za mbolea kwa msimu wa kilimo 2022/2023 ambapo isingekuwa mbolea za mbolea kiasi hicho kisingefikiwa kutokana na bei ya mbolea kuwa juu kwenye soko la dunia.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dkt. Batilda S. Burian alipokuwa akizungumza na ujumbe kutoka Mamlaka ya udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ukiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ruzuku, Louis Kasera ofisini kwake.
Balozi Dkt. Batilda amepongeza uamuzi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuinua Sekta ya Kilimo kwa kutoa ruzuku ya pembejeo pamoja na kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji.
"Kusema kweli bila hiyo ruzuku kiwango hicho kisingefika na wakulima wengi wameweza kupunguza gharama kubwa sana wasingepata mbolea ya ruzuku gharama ingekuwa ni mara mbili" Balozi Dkt. Batilda aliongeza.
Ameeleza kuwa, mkoa wake umejipanga kuhakikisha wakulima wanahakikiwa na kusajili wakulima ambao walikuwa hawajasajiliwa kwa msimu wa kilimo unaoishia.
Balozi Dkt. Batilda ametoa wito kwa wakulima kujitokeza kujihakiki na wale ambao hawajasajiliwa wakasajiliwe maana muda ndio huu
"Niwaombe sana wananchi wa Tabora vitabu vipo mjitokeze mkahakiki taarifa zenu kwa kipindi hiki cha wiki moja ili kuweka takwimu zenu vizuri ili baadaye asianze kulalamika na wale ambao hamkusajiliwa muda ndio huu" Balozi Dkt. Batilda alisisitiza.
Aidha, aliishukuru Wizara ya Kilimo pamoja na TFRA kwa kuanza maandalizi ya msimu ujao wa kilimo mapema na kueleza kuwa msimu unaoishia bado wengine hawajavuna hivyo wamepewa muda wa kutosha kujiandaa.
Naye Happiness Nnko, Afisa Kilimo wa manispaa ya Tabora ameeleza kuwa mfumo wa ruzuku haubagui mazao wakulima wananufaika kwa mazao yote na wakulima watapata mbolea kwenye maeneo yao.
Happiness ameeleza kufurahishwa na maamuzi ya Serikali ya kuvihusisha vyama vya ushirika katika suala zima la usambazaji wa mbolea na kueleza uamuzi huo utasaidia sana katika kupunguza changamoto zilizojitokeza msimu uliopita wa kilimo ikiwemo ya wakulima kufuata mbolea maeneo ya mbali.
No comments:
Post a Comment