Maafisa wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) wakitoa mafunzo kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA kwa wananchi zaidi ya 600 wa Halmashauri ya Wilaya Songea waliyofanyika Juni 3, 2023 Peramiho, Songea. Katika mafunzo hayo Msajili Msaidizi Bi. Fatma Jumanne ameelezea mchakato mzima wa kusajili Majina na Biashara na Kampuni, ambapo Afisa Leseni Bw. Koyan Ndalway ametoa elimu kuhusu hatua zinazohitajika ili kupata Leseni za Biashara kundi "A" na umuhimu wa kupata Leseni za Viwanda pamoja na usajili wa Viwanda Vidogo, huku Afisa Sheria Bw. Andrew Malesi akiwaleza juu ya umuhimu wa kusajili Alama za Biashara na huduma ili bidhaa zao ziweze kujitofautisha sokoni.
Na Mwandishi wetu Peramiho,Ruvuma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) na Mbunge wa Jimbo la Perahimo, Mhe. Jenista Mhagama, amewataka wananchi wa Jimbo hilo kurasimisha biashara zao ili kwenda na wakati na kujiletea maendeleo ya uhakika.
Waziri Mhagama ameyasema hayo wakati wa kuhitimisha mafunzo ya siku moja kwa wananchi wa Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma, yaliyotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), June 3, 2023.
Mhe. Mhagama amesema kuwa wananchi wa Songea kwa ujumla wamekuwa wakijishughulisha na kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi, hivyo kutokuramisha
biashara zao BRELA kunasababisha kukosa manufaa mengi zaidi.
Mhe. Mhagama ametumia fursa hiyo pia kuipongeza BRELA kwa kufanikisha mafunzo kuhusu huduma inazozitoa kwani wamekuwa lango la kufungua biashara nchini, hivyo wananchi wa Peramiho watanufaika na elimu hiyo.
" Niwapongeze BRELA mmefanya jambo zuri sana kufika katika eneo hili na kukutana na wananchi hawa na inaonesha wameelewa na watafanyia kazi, hivyo BRELA tutawahitaji wakati mwingine mje msajili hapa hapa watu wapate vyeti vyao, naomba salamu hizi mzifikishe kwa Afisa Mtendaji Mkuu na tunashukuru sana sisi wana Peramiho", ameongeza Waziri Mhagama.
Wakati huo huo Waziri Mhagama amewakumbusha wananchi kuchangamkia fursa ya mafunzo hayo kwa kuanza mchakato wa kujisajili BRELA ili kupata manufaa zaidi.
"Hili ni kwenu wananchi elimu hii ambayo ni muhimu muifanyie kazi na hakika mtaona manufaa yake kwani sisi ni wazalishaji wazuri wa mahindi na tunafanya biashara, hivyo tukisajili itakuwa rahisi hata kufanya biashara na mataifa mengine", ameongeza Waziri Mhagama.
Mafunzo hayo ya siku moja yamewakutanisha wananchi zaidi ya 600 kutoka katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea ambayo yameratibiwa na BRELA pamoja na Ofisi ya Mbunge wa Peramiho.
No comments:
Post a Comment