Wizara ya Habari, eGA Wawanoa Maafisa Habari Uingizaji Taarifa Tovuti Kuu ya Serikali - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, June 23, 2023

Wizara ya Habari, eGA Wawanoa Maafisa Habari Uingizaji Taarifa Tovuti Kuu ya Serikali


Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Idara ya Habari - MAELEZO kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), wametoa mafunzo ya uingizaji wa taarifa katika Tovuti Kuu ya Serikali kwa Maafisa Habari wa Vitengo vya Mawasiliano Serikalini vya Wizara.


Mafunzo hayo yaliyoanza Juni 22, 2023 jijini Mwanza yanaendelea kutolewa hadi Juni 24, 2023 ambapo Maafisa Habari wataelekezwa namna ya kuingiza taarifa mbalimbali za wizara na taasisi zilizo chini yao zikiwemo za bidhaa na huduma mtandao, namba za dharura, orodha ya taasisi pamoja na kuweka viunganishi vya tovuti za Serikali zilizopo kwenye kila wizara.


Akizungumza wakati akitoa mafunzo hayo, Mkufunzi ambaye pia ni Afisa Habari kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao, Rainer Budodi amesema kuwa, Maafisa Habari ndio wana jukumu la kutoa taarifa mbalimbali za Serikali hivyo, kwa kuwa Tovuti Kuu ya Serikali ni moja ya nyenzo muhimu ya utoaji taarifa ndani na nje ya nchi, kuna umuhimu wa wao kupatiwa mafunzo hayo ili wawe na uwezo wa kuweka taarifa katika tovuti hiyo.



"Tovuti hii ni msaada mkubwa kwa wanaohitaji kuifahamu Tanzania hasa wageni kutoka nchi za nje, hivyo tunatoa mafunzo kwa Maafisa Habari hawa ili waweke taarifa muhimu za Serikali zitakazowasaidia watu kuifahamu vizuri nchi yetu na kupata huduma kwa urahisi wakiwa huko huko nchini kwao kupitia huduma mtandao zilizowekwa katika tovuti hii,” alisema Budodi.


Kwa upande wake Afisa Habari kutoka Idara ya Habari - MAELEZO, Lilian Lundo amesisitiza Maafisa Habari kuendelea kuweka taarifa hizo hata baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo kwani mabadiliko Serikalini ni jambo lisiloepukika hivyo nao wanatakiwa kuendelea kufanya maboresho ya taarifa zao kila wakati.


Akizungumza baada ya kupata mafunzo hayo, Afisa Habari wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Sixmund Begashe amesema kuwa uwekaji wa taarifa katika tovuti hiyo ni daraja muhimu la kuusaidia Umma kidijitali kuzielewa huduma zinazotolewa na Serikali.


Tovuti Kuu ya Serikali ilianzishwa mwaka 2012 na kuboreshwa mwaka 2022 ambapo imebuniwa, kusanifiwa na kutengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) na upande wa maudhui unasimamiwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari chini ya Idara ya Habari - MAELEZO.


Lengo la kuanzishwa tovuti hiyo ni kuwa na dirisha moja la kutoa taarifa na huduma zinazotolewa na Serikali.

No comments:

Post a Comment