Na: James Mwanamyoto (OR-TAMISEMI)
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Serikali ya Awamu ya Sita katika Mwaka wa Fedha 2022/23 ilitenga bilioni 3.2 zilizoiwezesha TARURA kujenga barabara za kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita 51.28 mkoani Njombe.
Mhe. Ndejembi amesema hayo akiwa katika Halmashauri ya Mji Makambako, mara baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango kumpatia fursa ya kuzungumza na wakazi wa eneo hilo.
Mhe. Ndejembi amesema, kabla Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani TARURA ilitengewa shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa barabara mkoani Njombe, na kuongeza kuwa Mhe. Rais aliongeza bajeti iliyofikia shilingi bilioni 3.2 ili kuongeza wigo wa ujenzi wa barabara mkoani humo.
“Mhe. Makamu wa Rais katika kilomita 51.28 za barabara zilizojengwa mkoani Njombe wananchi wa hapa Makambako wamenuifa na kilomita 12 zilizojengwa katika mji huu wa Makambako,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, katika mwaka huu wa fedha 2023/24 Serikali imetenga bilioni 1 kwa ajili ya kujenga barabara za kiwango cha lami ambazo zitawekewa taa katika Halmashauri ya Mji wa Makambako.
Aidha, Mhe. Ndejembi amesema katika mwaka wa fedha 2021/22 Halmashauri ya Mji wa Makambako ilipokea zaidi ya shilingi milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Kitisi.
Sanjali na hilo, Mhe. Ndejembi amesema katika kata ya Kitandililo Serikali imeleta milioni 583 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Sekondari na inaendelea na ujenzi wa kituo cha afya ambacho kimetengewa milioni 250 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wake.
No comments:
Post a Comment