Katibu Mkuu Ndunguru akoshwa na Proramu ya Mifumo Serikalini - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, July 4, 2023

Katibu Mkuu Ndunguru akoshwa na Proramu ya Mifumo Serikalini

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Adolf Ndunguru akifungua kikao kazi cha kutambua mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa Programu ya Mifumo katika Sekta ya Umma Jijini Dodoma.
Dkt. Emmanuel Malangalila ambaye ni Mkurugenzi wa Programu ya Kuimarisha Mifumo ya Usimamizi katika Sekta ya Umma – Public Sector Systems Strengthening PS3+ akitoa maelezo ya awali kuhusu mafanikio na changamoto za Mifumo ya TEHAMA Serikalini inayofadhiliwa na Programu ya PS3+
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi cha kupitia mafanikio na changamoto za Mifumo Serikalini ambao ni Makatibu Tawala Mikoa, Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa Sehemu ya Usimamizi, Ufuatiliaji na Ukaguzi – Management Monitoring and Inspection (MIMI) na Wataalamu wa TEHAMA wa Mikoa kinachoendelea Jijini Dodoma.


Na Fred Kibano, Dodoma


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Adolf Ndunguru amefungua kikao kazi cha kutambua mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa Programu ya Mifumo katika Sekta ya Umma na kusifu utekelezaji wake.  


Akifungua kikao kazi hicho mapema leo tarehe 03 Julai, 2023 katika ukumbi wa Mtakatifu Gaspar Jijini Dodoma Katibu Mkuu Ndunguru amesema baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni kuwawezesha Maafisa wa Halmashauri kuandaa taarifa nzuri za fedha na kupelekea Mamlaka hizo kupata Hati Safi pamoja na kuimarika mifumo ya sekta ya afya.


 “uboreshaji wa Mfumo wa usimamizi wa utoaji wa huduma kwenye vituo vya kutolea huduma za afya (GoTHoMIS) umezuia upotevu wa dawa na vifaa tiba, kudhibiti na kuongeza makusanyo ya ada ya kuchangia huduma na pia ubadilishanaji na utoaji wa taarifa kwa wakati, uwepo wa mfumo wa uandaaji wa mipango, bajeti na utoaji wa taarifa wa PlanRep umepunguza gharama za machapisho ya nyaraka mbalimbali” amesema ndunguru.


Akitoa maelezo ya awali Dkt. Emmanuel Malangalila ambaye ni Mkurugenzi wa Programu ya Kuimarisha Mifumo ya Usimamizi katika Sekta ya Umma – Public Sector Systems Strengthening PS3+ amesema Mradi huo wa Kuimarisha Mifumo Serikalini ni wa miaka 10 na ulianza mwaka 2015 na utakamilika mwaka 2025 na matarajio ya mradi kwa upande wa wahisani ni kuona unaendelezwa katika ngazi zote ambazo ni Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mikoa na Halmashauri ambazo zote zimeanza kuutekeleza.


Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Toba Nguvina ametoa rai kwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Programu ya Kuimarisha Mifumo ya Usimamizi katika Sekta ya Umma (PS3+) kuifanya mifumo mingi zaidi kuwasiliana ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa takwimu kama vile mtu ambaye yupo mkoani aweze kuona au kupata taarifa za zahanati moja kwa moja badala ya kutumia Maafisa kufuata taarifa za zahanati moja hadi nyingine ili kuongeza ufanisi zaidi katika utendaji. 


Kikao kazi hicho cha siku mbili kimefadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Mradi wa PS3+ na kina lengo la kuweka mikakati ya uendelevu katika Mifumo ya Usimamizi katika Sekta ya Umma kilichowahusisha Makatibu Tawala Mikoa, Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa Sehemu ya Usimamizi, Ufuatiliaji na Ukaguzi – Management Monitoring and Inspection (MIMI) na Wataalamu wa TEHAMA wa Mikoa.

No comments:

Post a Comment