MADINI YACHAGIZA MAENDELEO SEKTA YA AFYA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, July 4, 2023

MADINI YACHAGIZA MAENDELEO SEKTA YA AFYA


Na Mwandishi wetu-Shinyanga

Katika kuifungamanisha Sekta ya Madini na sekta nyingine, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amekabidhi kwa Serikali Zahanati, Nyumba ya Mganga Mkuu na Gari la kubebea wagonjwa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 312.5.


Makabidhiano hayo yamefanyika katika Kijiji cha Nyamishiga kilichopo Kata ya Lunguya katika Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga baada ya Kikundi cha Mshikamano kilicho chini ya Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake (TAWOMA) kutoa mchango huo kwa Serikali kama mchango wake kwa jamii katika maeneo yanayokuzunguka mgodi.


Aidha, Dkt. Biteko ameipongeza TAWOMA kwa kuchangia maendeleo katika Sekta ya Afya na kuwataka waendelee kutoa mchango zaidi katika huduma mbalimbali za kijamii na kutoa wito kwa wamiliki wengine wa leseni kuchangia maendeleo katika jamii zinazowazunguka shughuli za madini.


Pamoja na mambo mengine, Dkt. Biteko amewataka wachimbaji wadogo wa madini nchini kuungana, kupendana na kushirikiana ili kufanya shughuli zao kwa amani na upendo.


Naye, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme amekishukuru Chama cha Wachimbaji Wadogo Wanawake kwa kuona umuhimu wa kuchangia maendeleo ya jamii katika eneo wanalofanyia shughuli zao za uchimbaji madini.


Mndeme amewataka Wanawake kuendelea kuchapa kazi kwa lengo la kujiletea maendeleo na ametoa wito kwa wanawake wote nchini kuchangamkia fursa zilizopo katika Sekta ya Madini ili kuongeza kipato na kuepuka kuwa tegemezi.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAWOMA Semeni Malale amesema Kikundi cha Mshikamano TAWOMA kimechangia zaidi ya Shilingi milioni 289 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Zahanati, jengo la nyumba ya Mganga Mkuu na Ununuzi wa gari la kubebea wagonjwa wa dharura katika kijiji cha Nyamishiga.


Malale amemshukuru Waziri Biteko kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa Zahanati hiyo ambayo itapelekea kupunguza changamoto kwa wananchi wa kijiji hicho ambao hufuata huduma za afya umbali mrefu.


Ziara hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Chama cha Mapinduzi (CCM) na TAWOMA akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Kaimu Kamishna wa Madini Msechu Maruvuko, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Kahama Jeremia Hango, Mwenyekiti wa TAWOMA Taifa Semeni Malale na Katibu Mkuu wa TAWOMA Salma Ernest.

No comments:

Post a Comment