Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi- Dar es salaam
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura anapenda kuwakaribisha wananchi wote katika ufunguzi wa Mkutano wa Mafunzo wa Jumuiya ya Askari Polisi wa Kike wa Duniani Ukanda wa Afrika (IAWP - International Association of Women Police - African Chapter) utakaofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam Julai 23, 2023 kuanzia Saa Tatu kamili Asubuhi.
Akitoa taarifa hiyo msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini Kamishna msadizi Mwandamizi SACP David Misime amesema Mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano huo anatarajiwa kuwa Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na utahudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo Viongozi wa Serikali, Mabalozi, Viongozi wa Dini, Mashirika yasiyo ya Kiserikali pamoja na Wajasiriamali.
Ameleza kuwa Washiriki wa mkutano huo kutoka nje ya Tanzania ambao wamethibitisha kushiriki ni kutoka katika nchi za Afrika Kusini, Botswana, Ethiopia, Ghana, Kenya, Malawi, Nigeria, Sierra Leone na Zimbabwe. Wengi wao wameshawasili na wengine wanaendelea kuwasili.
Misime pia amebainisha kuwa upande wa Tanzania washiriki wanatoka Jeshi la Polisi Tanzania, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Jeshi la Magereza, Jeshi la Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mahakama, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA), Waendesha Mashtaka, Wanasheria wa Serikali, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Watumishi raia wa Jeshi la Polisi Tanzania pamoja na wake wa Askari wa Jeshi la Polisi Tanzania.
Mwisho amewambia waandishi wahabari kuwa Maandalizi yote ya mkutano huo wa mafunzo yameshakamilika ambapo zaidi ya washiriki 2,000 kutoka ndani na nje ya Tanzania watashiriki. Katika ufunguzi huo kutakuwa na maonesho na burudani mbalimbali.
No comments:
Post a Comment