Naibu Katibu Mkuu atoa maagizo mazito kwa mkandarasi. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, July 23, 2023

Naibu Katibu Mkuu atoa maagizo mazito kwa mkandarasi.


Na Mwandishi wetu -Shinyanga

Naibu katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Cyprian Luhemeja amemtaka Mkandarasi Kampuni ya PET Cooperation kuripoti kwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama bila kukosa siku ya jumatatu Tarehe 24 Julai, 2023.


Mhandisi Luhemeja amechukua hatua hii baada ya Mkandarasi huyo kushindwa kukamilisha utekelezaji wa mradi wa maji unaohusisha vijiji vitatu vya Mwazinga, Mwaningi na Burige wilayani Msalala mkoa wa Shinyanga wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.2.


"Nitoe maagizo kwa Mkandarasi kampuni ya PET, ifikapo jumatatu aripoti ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa taratibu zaidi kuhusu mradi huu, hatuwezi kuvumilia Mkandarasi kulipwa malipo ya awali ya shilingi milioni 366 na asionekane tena, hii haivumiliki" Mhandisi Luhemeja amesema



Ameongeza kuwa wakandarasi wenye tabia hii ni kikwazo katika miradi ya maji na wanarudisha nyuma juhudi za Serikali kwa kampuni za wazawa kuaminika na kupewa kipaumbele kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.


"Nitoe agizo kwa Meneja wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga, kuwasiliana na wanasheria wa Wizara ya Maji na kuanza mchakato wa kuvunja mkataba kwa Mkandarasi huyu, lakini pia Mkandarasi huyu arudishe fedha yote ya Serikali aliyolipwa kama malipo ya awali" Mhandisi Luhemeja amefafanua.


Meneja wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Julieth Payovela ameeleza kuwa kwa hali ilivyo ni dhahiri Mkandarasi ameshindwa kazi kwani kila mara wanapowasiliana nae kwa ajili ya mazungumzo hatoi ushirikiano.


Kusuasua kwa mradi huu kumesababisha adha ya upatikanaji huduma ya maji kwa wakazi wa vijiji hivyo ambao ndio wanufaika wakuu kama Serikali ilivyopanga.

No comments:

Post a Comment