Na Mwandishi wetu-Tanga
Shehena za Mizigo zinazohudumiwa kupitia Bandari ya Tanga kwenda maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi zimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 8.2 kwa kipindi cha miezi sita kuanzia January mpaka Juni, 2023
Akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Kamati ya Maboresho ya Huduma za Bandari kwa bandari ya Tanga mkoani humo kwa niaba ya Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Huduma za Usafiri kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi-Sekta ya Uchukuzi Mhandisi Aron Kisaka amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilitoa fedha kwa ajili ya kufanya maboresho makubwa kwenye Bandari ya Tanga ikiwemo kuongeza kina,magati na miundombinu ya Reli inayoingia Bandarini hapo ,kufungwa kwa mitambo mipya ya kupakia na kupakua makasha ambavyo vimechangia kuongeza shehena za mizigo kwa kuanza kuhudumiwa Meli kubwa kwenye Bandari hiyo.
Mha Kisaka amesema kwa kipindi cha miezi sita kuanzia mwezi Januari mpaka Juni, 2023 Bandari ya Tanga imeweza kuhudumia makasha 3,405 ya mizigo mbalimbali inayotoka na kwenda maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi yakiwemo makasha 141 ya shaba.
“Maboresho yaliyofanyika katika bandari hii yamechangia sana kuongeza uhudumiaji wa shehena za mizigo kwani yamesababisha muda wa meli kukaa bandarini kupungua kutoka siku 3 mpaka siku 0.8 hivyo kupunguza gharama za uendeshaji kwa watumiaji na kuvutia watumiaji zaidi na Meli kubwa kuanza kutia nanga bqandarini hapa” amesisitiza Mhandisi Kisaka
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga Bw. Peter Milanzi amesema Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepanga kuongeza gati mpya mbili kwa ajili ya kuendelea kuboresha huduma kwenye bandari ya Tanga ambapo gati ya kuhudumia makasha itajengwa upande wa mashariki mwa bandari na gati kwa ajili ya kuhudumia abiria wa kawaida pamoja na watalii wanaokuja kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vilivyomo mkoani Tanga litajengwa upande wa Magharibi ambapo utekelezaji wake utaanza mwaka huu wa fedha 2023-2024.
Naye Mdau wa Bandari nchini Bi Lilian Mbwambo kutoka Tanga Modern Clearing and Forwading company amesema mikutano ya aina hii inayowakutanisha wadau wa bandari imekuwa na tija kubwa kwa watumiaji kwani inajenga uelewa wa pamoja na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili watumiaji na kupatiwa ufumbuzi na hii imekuwa ikivutia wawekezaji zaidi nchini na kupelekea uongezekaji wa shehena za mizigo kwani mizigo mikubwa karibu yote husafirishwa kwa njia ya maji.
Mikutano ya Maboresho ya Huduma za Bandari inayowakutanisha wadau wa Bandari Nchini kote chini ya usimamizi wa TPA hufanyika mara moja kila mwezi kwa lengo la kujadili ubora wa huduma zinazotolewa na Bandari zetu,changamoto zinazojitokeza na kupatiwa ufumbuzi ili kuongeza ufanisi wa bandari Nchini kote na kuongeza pato la Taifa.
No comments:
Post a Comment