Na Mwandishi wetu-Tanga
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Wakili Mnyema, ameeleza uwepo wa changamoto ya wakulima mkoani humo kusita kutumia mbolea za viwandani kwenye shughuli za kilimo kutokana na imani kuwa mbolea inaharibu aridhi.
Ametoa wito kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuendelea kushirikiana na ofisi yake katika kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kwa wananchi wa mkoa huo ili waongeze tija kwenye uzalishaji.
Mnyema amesema hayo tarehe 18 Julai, 2023 ofisini kwake alipokuwa akizungumza na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya TFRA na Menejimenti waliofika kueleza uwepo wao wenye lengo la kutembelea wazalishaji wa mbolea na visaidizi vya mbolea waliopo mkoani hapo.
‘‘Ni Bodi mpya lakini mmeanza na kasi kubwa katika kusimamia tasnia ya mbolea’’aliongeza Myema.
Kuna vitu vingi kama mkoa tumevipokea ikiwemo Wakuu wa Wilaya, makatibu Tawala ndani ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mengi yamefanyika nasi tunaendelea kuvasemea kwa wananchi na hata suala hili la kutoa ruzuku kwenye mbolea tutalisemea ili wananchi wajue jinsi Mama alivyowekeza kwenye kilimo, alimaliza.
Akikazia maneno ya Katibu Tawala Mnyema Mkurugenzi wa Bodi ya TFRA Thobias Mwesigwa amesema, elimu ya umuhimu wa matumizi ya mbolea unaeleweka zaidi kwa wamiliki wa viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo lakini watumiaji hawana elimu hiyo na hivyo kupelekea mwitikio mdogo wa kutumia mbolea kwenye kilimo.
Aliahidi kuifanyia kazi changamoto hiyo kwa kuweka mikakati ya kuhakikisha wazalishaji, Menejimenti na Ofisi za mikoa zinashirikiana katika kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea.
"Tumelichukua na tutalifanyia kazi kwenye vikao vyetu vya kiutendaji" Mwesigwa alisisitiza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Dkt. Shimo Peter Shimo amesema agenda ya mbolea ni agenda iliyopewa kipaumbele kikubwa sana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na kutoa wito kwa viongozi wa mikoa, wilaya mpaka ngazi za chini za serikali kuzungumzia kila wanapokuwa na vikao na wananchi.
Amesema kuzungumzia jambo hilo kutawafanya wananchi kuhamasika na kuiona kwa mapana thamani wanayopewa na viongozi wa nchi katika kuhakikisha wanajikwamua kiuchumi.
Naye Mkurugenzi Hadija Jabiri ameiomba serikali kuendelea kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya mbolea katika Mkoa wa Tanga na kueleza uzalishaji ukiwa ni mkubwa utasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa mbolea nchini na kupunguza utegemezi wa kuagiza mbolea nje ya nchi.
Akizungumza katika kikao hicho Gothard Liampawe Meneja wa TFRA Kanda ya Kaskazini amesema pamoja na Mkoa wa Tanga kuongoza kwa kuwa na viwanda vingi vya uzalishaji wa mbolea na visaidizi vya mbolea, bado mkoa huo umekuwa changamoto kwenye matumizi ya mbolea pamoja na elimu inayoendelea kutolewa.
Amesema TFRA imejitahidi kuondoa changamoto ya usambazaji wa mbolea iliyojitokeza msimu wa kilimo wa 2022/2023 KWA kuvitumia vyama vya ushirika vilivyotayari kushiriki katika kusambaza mbolea na tayari vyama hivyo vimepewa mafunzo ya uuzaji wa mbolea kwa kwa kutumia mfumo wa kidigitali ulioboreshwa.
Wajumbe haowalitembelea viwanda viwili vya uzalishaji wa mbolea na visaidizi vya mbolea ikiwa ni Neelkanth Chemmicals LTD na ABM na kushauriana namna bora ya kuhamasisha matumizi ya bidhaa wanazozizalisha Pamoja na kuheshimu Kanuni, Sheria na miongozo inayosimamia tasnia ya mbolea nchini.
No comments:
Post a Comment