WAKUFUNZI WA SOMO LA HISABATI WAJENGEWA UWEZO KUFUNDISHA KWA KUTUMIA TEHAMA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, July 11, 2023

WAKUFUNZI WA SOMO LA HISABATI WAJENGEWA UWEZO KUFUNDISHA KWA KUTUMIA TEHAMA.


Na Mwandishi wetu Morogoro

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imedhamiria kuondoa changamoto ya ufundishaji wa somo la Hisabati kwa kuendesha mafunzo kazini kwa Wakufunzi wa somo hilo kutoka Vyuo vya Ualimu vya Serikali juu ya ufundishaji ili kuwapa mbinu bora na mahiri za kufundisha kwa kutumia TEHAMA.


Akifungua mafunzo hayo Mkoani Morogoro Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema mafunzo hayo yanalenga pia kuwapa uwezo wakufunzi kuwezesheshana kumudu somo hilo hususan kwa njia ya mtandao kupitia kituo cha Umahiri cha Hisabati kilichopo katika Chuo cha Ualimu Morogoro ambacho ni mahsusi kuwahudumia wakufunzi na walimu wa somo la hisabati nchini.


Amesema kumekuwa na changamoto ya ufundishaji wa somo la Hisabati na kuwafanya wanafunzi kutopenda somo hilo na ndio maana Serikali imefanya mafunzo kwa wakufunzi ili kuwapa mbinu za kufundisha kwa kutumia TEHAMA ili kuvutia wanafunzi kupenda kusoma somo hilo.


“Tafiti zimeonesha wanafunzi wengi hawavutiwi kusoma somo la Hisabati na ufaulu kuwa mdogo pengine ni kutokana na namna somo hili linavyofundishwa hivyo mafunzo haya yatawapa mbinu ya bora za kufundisha na kuwafanya wanafunzi kuelewa na kupenda somo hilo na niseme tu mafunzo haya yahusishe pia wakufunzi kutoka Vyuo vya Ualimu vya binafsi kwa kuwa wanafundisha watoto wa kitanzania kuwa walimu ,”amesema Prof. Nombo.


Na kuongeza “Tunajua hisabati inatumika katika maisha ya kila siku tunataka wakufunzi hawa waweze kuwezesha walimu tarajali ambao watafundisha msingi na sekondari kutumia hisabati katika maisha ya kila siku lakini kuwezesha wanafunzi kufaulu.



Prof. Nombo amesema utoaji wa mafunzo hayo ni mwendelezo wa mikakati ya Wizara iliyojiwekea kuhakikisha hakuna changamoto za ufundishaji wa somo hilo na hatimaye wanafunzi kupenda kusoma somo hilo.


“Pamoja na kutoa mafunzo kazini tunatoa pia ufadhili wa masomo (Samia Scholarship) kwa wanafunzi wanaofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi wanaomaliza kidato cha sita na kuchagua kuendelea na masomo ya sayansi katika fani za tiba, uhandisi na sayansi".


Amesisitiza kuwa Serikali inaendelea na mikakati ya kuwavutia wasichana kupenda masomo ya sayansi na hisabati hivyo kuongeza wanafunzi wa kike watakaopenda kufundisha masomo.


Prof. Nombo amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuwekeza kwenye Sekta ya elimu ili kutoa elimu iliyo bora.


Aidha ameishukuru Serikali ya Canada kupitia Mradi wa TESP kwa mchango wao mkubwa katika kuendeleza Elimu ya Ualimu nchini kwa kuboresha miundombinu ya Vyuo vya Ualimu, utoaji wa mafunzo kazini kwa walimu na utaoji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.


Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa mafunzo ya Ualimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Huruma Mageni amesema jumla ya wakufunzi 155 wamepatiwa mafunzo hayo


Ameongeza kuwa mafunzo yanatolewa katika chuo cha Ualimu Morogoro kwa kuwa Serikali imeanzisha kituo cha umahiri cha hisabati ili kuimarisha na kuendeleza mafunzo ya ufundishaji wa somo hilo katika chuo hicho.


Nae Mratibu wa Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (TESP) Cosmas Mahenge amesema Mradi umewekeza kwenye masuala ya TEHAMA katika vyuo vya ualimu na sasa unatoa mafunzo ya mbinu za ufundishaji wa somo la Hisabati kwa kutumia TEHAMA ili waendane na mabadiliko yalipo.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakufunzi walioshiriki mafunzo hayo wamesema yatawaimarisha katika ufundishaji hususani matumizi ya TEHAMA na kufanya walimu tarajali wapende somo la hisabati.

No comments:

Post a Comment