Na WJJWM, DSM
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amefungua Warsha ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) ambapo ametoa wito kwa taasisi hiyo kushirikiana na Serikali katika kuwainua wanawake kiuchumi na kutokomeza ukatili wa kijinsia katika jamii.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo, Julai 03, 2023 wakati akifungua warsha ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO) ukumbi wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Dar es Salaam ambapo wajumbe kutoka nchi mbalimbali za Afrika wameshiriki ufunguzi huo.
"Warsha hii imelenga kukuza usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili na unyanyasaji kwa wanawake na inawapa nafasi kubwa ya kujifunza na kushirikishana mbinu za kukabiliana na changamoto hizo kwa kuwa na sauti ya pamoja.
"Jambo hili ni jema kwani siku zote umoja unaleta matunda chanya na ya haraka zaidi." amesema Dkt. Gwajima.
Dkt. Dorothy Gwajima ameongeza kuwa, amefarijika kwakuwa WAWATA pia ina lengo la kumfanya mwanamke ajitambue kuwa yeye ni muhimu ndani ya Jamii na maendeleo ya kiroho na kimwili.
Kwa upande wake Rais wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Afrika, World Union of Catholic Women Organization (WUCWO) na Mwenyekiti wa WAWATA, Eveline Ntenga amesema, kwenye vipaumbele nane vya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa bajeti ya mwaka 2023/24 vipo vipaumbele viwili vinavyoendana na Mradi wa World Women Observatory (WWO) ambavyo ni kuratibu hatua za kukuza usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake kiuchumi na kiungozi, kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, Watoto na wazee na kuratibu utoaji wa huduma za msingi kwa watu wenye mahitaji maalum.
Aidha Eveline ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii kuweka mkazo juu ya suala la kuwataka wazazi waone umuhimu wa watoto wa kike kupata elimu kwanza badala ya kufikiria kuwaozesha mapema.
Aidha Rais huyo ameiomba Wizara iwasaidie kuendelea kuweka utaratibu sahihi na wa haraka kuanzia ngazi ya Msingi ili kufikisha taarifa za unyanyasaji na ukatili zinazofanywa na jamii kwa makundi yote katika vyombo husika.
“Tunaomba zichukuliwe hatua kali na kwa haraka kwa wale wote wanaohusika na vitendo vya ukatili kwa makundi yote “ amesema Bi. Aveline.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Pd. Dkt. Charles Kitima, amesema katika kufikia maendeleo halisi kama ilivyolengwa kwenye ajenda ya maendeleo ya Dunia (Suistainable Development Goals) ya mwaka 2030, Kanisa linawaona wamama kama watendaji wakuu, na wakishikwa mkono na kanisa na Serikali wanaweza wakaifanya Dunia kuwa imara.
Dkt. Kitima amesema, jina la Wizara Wizara ya Maendeleo ya Jamii linasawidi mambo mengi yanayohusu utu wa mwanadamu ambapo ndipo Mungu Muumba anatukuka, Utukufu wa Mungu uko katika Utu wa mwanadamu, kwani wizara inashughulikia mambo ya Watoto, makundi yaliyotengwa, na akina mama hii ni heshima kubwa kwamba Waziri wa Wizara hii ni mama.
No comments:
Post a Comment