Kamati ya Bunge yaipa heko Wizara ya Maji - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, August 18, 2023

Kamati ya Bunge yaipa heko Wizara ya Maji


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeipongeza Wizara ya Maji kwa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia maelekezo mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa na kamati hiyo. Pongezi hizo zimetolewa leo Jijini Dodoma wakati Wizara hiyo ilipokuwa ikiwasilisha utekelezaji wa shughuli za Chuo cha Maji.


Mhe. Jackson Kiswaga (Mb) Mwenyekiti wa Kamati hiyo amesema Wizara ya Maji imekuwa sikivu katika kufanyia kazi maoni na maelekezo mbalimbali hivyo imeweza kupata mafanikio, ikiwamo maendeleo makubwa katika Chuo cha Maji.


Amesisitiza na kuwataka wahakikishe watumishi wa Sekta ya Maji wanaendelea na utaratibu huo ili kuleta mabadiliko chanya kwa Watanzania. 


Awali akiwasilisha taarifa ya chuo hicho kwa niaba ya Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) Mkuu wa Chuo cha Maji Dkt. Adam Karia amesema Chuo cha Maji kimekuwa na mafanikio anuwai ikiwemo ongezeko la watahiniwa pamoja na machapisho ya tafiti mbalimbali ambazo zimekuwa msaada mkubwa katika kukuza uchumi na kutoa majibu ya changamoto mbalimbali katika jamii.


 “ Katika kipindi cha miaka miwili kuanzia 2021/22 hadi 2022/23), Chuo kimedahili wanafunzi 1,727 katika ngazi ya Shahada (Degree), na 3,360 kwa ngazi ya stashahada (Diploma). 
 

Mwaka 2021/22, Chuo kilitoa jumla ya wahitimu wapatao 133 wa ngazi ya Shahada, 269 wa ngazi ya Stashahada, na 62 wa ngazi ya Cheti. Wataalamu hawa pamoja na wengine ambao wamekuwa wakizalishwa na chuo hiki wamekuwa msaada mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya maji na sekta nyingine mtambuka” Dkt. Karia Amesema 


Amesema ili kuendelea kuzalisha wataalamu wabobezi zaidi Chuo cha Maji kimeanzisha Shahada mbili za Uzamili (Masters Degree programs) ambazo zitaanza kutolewa mwaka 2023/24, Shahada hizo ni Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Rasilimali Maji na Huduma (Master Degree in Water Resources and Utility Management) pamoja na Shahada ya Uzamili ya Uhandisi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira (Master Degree in Water Supply and Sanitation Engineering)


Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) akiongea katika kikao hicho ameihakikishia kamati ya Bunge kuendelea kusimamia maagizo yote yanayotolewa ili chuo kiwe mfano bora katika vyuo barani Afrika.


Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba ameahidi kuendelea kusimamia nidhamu ya utekelezaji wa maagizo yanayotolewa na viongozi wote na serikali kwa ujumla katika kuhakikisha chuo kinazalisha wataalamu wenye ujuzi, weledi na umahiri katika Sekta ya Maji.


Chuo cha Maji kilianzishwa mwaka 1974 kama kitengo ndani ya Wizara ya Maji ambapo kimechangia kuzalisha nguvu ya rasilimaliwatu inayotumika katika Sekta ya Maji hapa nchini na nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment