MABORESHO YALIYOFANYIKA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA DODOMA YAIMARISHA UTOAJI WA HUDUMA-DKT.IBENZI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, August 9, 2023

MABORESHO YALIYOFANYIKA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA DODOMA YAIMARISHA UTOAJI WA HUDUMA-DKT.IBENZI


Na Okuly Julius-Dodoma

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imefanya mabadiliko makubwa katika uboreshaji wa jengo la dharura katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma , ambapo wagonjwa 34 wanapata huduma za uchunguzi, vipimo na malipo ya huduma kwa wakati mmoja na uharaka zaidi kulinganisha na hapo awali wagonjwa wanne tu.


Hayo yameelezwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt.Ernest Ibenzi wakati akizungumza na waandishi wa Habari leo Agosti 9,2023,Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji na vipaumbele vya Hospitali hiyo katika mwaka wa fedha wa 2023/2024.



"Kabla ya ujenzi wa jengo jipya la dharura tulikuwa tunahudumia wagonjwa wanne tu kwa wakati mmoja ila sasa mambo yamebadilika sana mara baada ya maboresho makubwa yaliyofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na kwa sasa wagonjwa 34 wanapata huduma za uchunguzi, vipimo na malipo ya huduma kwa wakati mmoja na uharaka zaidi,"amesema Dkt.Ibenzi




Pia Dkt.Ibenzi amesema kuwa maboresho mengine yaliyofanyika katika Jengo la kuwahudumia wagonjwa walio kwenye uangalizi maalum (ICU ambapo Kwa sasa lina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 38 ukilinganisha na wagonjwa wa 3 waliohudumiwa katika jengo la zamani, na lina vifaa vya kisasa ikiwemo vitanda vyote kuwageuza wagonjwa kwa kutumia umeme.


Mganga Mfawidhi huyo ameongeza kuwa Hospitali hiyo imesimika mtambo wa gesi tiba ya hewa ya oksijeni ambapo vitanda 297 vimeunganishwa na hewa hiyo, hii inasaidia kupunguza gharama za ununuaji wa gesi tiba ya hewa ya oksijeni, pia hospitali inaongeza kipato kutokana na kuuza gesi hii kwa Taasisi nyingine za afya.



" Kati ya ukarabati na ujenzi unaofanyika kwa sasa ni pamoja na jengo la watoto ili kukabiliana na changamoto ya watoto kulala kwa kubanana na nakanusha kuwa hakuna malipo anayopatiwa daktari tofauti na mshahara wa Serikali wa mwisho wa mwezi ili aweze kutoa huduma kwa wagonjwa,"amesisitiza Dkt.Ibenzi


Ambapo Dkt.Ibenzi amesema kuwa Kwa siku Hospitali ya Rufaa ya Dodoma inapokea wagonjwa zaidi ya 1,500 na hospitali ina uwezo wa kulaza wagonjwa 250 hadi 350 kwa wakati mmoja.


Katika mwaka huu wa fedha wa 2023/2024 Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma imetengewa Shilingi bilioni 24 ili iendelea kuwahudumia wananchi kwa wakati na huduma bora kwa gharama ndogo, kutumia muda mfupi katika kumuhudumia mgonjwa pamoja na uhakika wa dawa za kutosha na kuendelea kukarabati na kujenga majengo kwa ajili ya kutolea huduma mbalimbali za afya.




SHUGHULIMBALIMBALI ZILIZOTEKELEZWA NA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA DODOMA KATIKA KIPINDI CHA MWAKA 2022/2023.


Kwa kipindi cha mwaka mzima 2022/2023 Idara ya magonjwa ya nje na dharura ilihudumia wagonjwa 251,174, wagonjwa 13,607 walikuja kwa utaratibu wa rufaa, 120,263 (48%) walitibiwa kwa bima ya NHIF, 8,174 (3%) walikuwa wa bima nyingine, 16,896 (7%) walikuwa wa CHF, na 105,841(42%) walipata huduma kwa njia nyingine za uchangiaji ikiwemo wa msamaha. Aidha wagonjwa 32,090 walilazwa.


Kwa kipindi cha mwaka mmoja yaani 2022/2023 Hospitali ilifanikiwa kufanya Kliniki tembezi katika maeneo tofauti ndani ya Mkoa wa Dodoma ambapo wagonjwa 552 walihudumiwa.


Katika kipindi cha mwaka 2022/2023 Idara ya Macho ilifanikiwa kutoa huduma kwa wagonjwa 5,319, wagonjwa waliofanyiwa upasuaji 2,234, wagonjwa 843 walipatiwa dawa.


Kwa mwaka 2022/2023 Idara ya famasia imehudumia jumla ya wagonjwa 183,664, kati yao wagonjwa 83,583 walikuwa wa Bima na 100,081 wa kujitegemea.


Wastani wa mahitaji ya damu kwa mwaka Hospitali ya Rufaa ya Dododma ni chupa/units 5,400, kipindi cha mwaka 2022/2023 chupa/Units 5,368 zilikusanywa sawa na asilimia 99% aidha, hakuna mteja aliyekosa damu.


Kitengo cha uchunguzi kwa njia ya mionzi (Radiolojia) kwa mwaka 2022/2023 kilifanikiwa kufanya jumla ya vipimo 37,975 vya aina mbalimbali.


Hospitali imefanikiwa kununua vifaa tiba vya kisasa ikiwemo; CT- Scan, X- Ray mashine 3 za kisasa zaidi kutoka mashine 1, mashine za Ultrasound 4, mashine za kisasa za maabara na vitendanishi, tunafanya vipimo 136 vinavyosaidia wananchi kutambua changamoto mbalimbali za afya zao.


Hospitali ina vyumba 12 vya kufanyia upasuaji ‘oparesheni’ na kwa siku takribani wagonjwa 70 wanafanyiwa oparesheni.


Hospitali ilikuwa na ufinyu wa jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje na dharura ambalo lilikuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 4 tu wa dharura kwa wakati mmoja.

No comments:

Post a Comment