Na Okuly Julius-Dodoma
Mhagama amesema kutokana na taarifa ya Utabiri wa hali ya hewa ya taarehe 24 Agosti, 2023,iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) iliyotoa mwelekeo wa mvua za msimu wa Vuli kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2023 kuonesha uwepo wa El-Niño itakayosababisha vipindi vya mvua kubwa kwa mwezi Oktoba mpaka Disemba 2023 na kuendelea mpaka Mwezi Januari 2024.
Mhagama ameyasema hayo leo Agosti 31,2023 Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kufuatia taarifa zilizotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) juu ya uwepo wa El-Niño wakati wa mvua za msimu wa Vuli kwa mwezi Oktoba mpaka Disemba 2023.
"Madhara yanayoweza kutokea katika sekta kutokana na uwepo wa El-Nino utakaosabisha mvua kubwa ni kama mafuriko kuharibu miundombinu, madhara ya kiafya, kiuchumi, kijamii na upotevu wa mali.
maporomoko ya ardhi kuathiri makazi, mazingira, mashamba, usafiri na shughuli zingine hususani uchimbaji madini,magonjwa ya milipuko kwa binadamu na wanyama na wadudu waharibifu wa mazao na mimea, amesema Mhagama
Pia Mhagama amezitaka kamati hizo kuainisha na kuandaa rasilimali za usimamizi wa maafa kwa kila sekta kushiriki kikamilifu katika eneo lake,kuandaa mipango ya kuzuia milipuko ya magonjwa kwa binadamu, wanyama na mimea,kuhifadhi mazingira na kulinda miundombinu ya barabara, maji, umeme na mawasiliano ili kupatikana huduma wakati wote,kuelimisha wananchi juu ya hatua za kuchukua tahadhari ili kuaokoa maisha na mali,kutoa taarifa kwa haraka kwa mamlaka husika kuhusu dalili za kutokea maafa na yanapotokea maafa,kuhama kwenye maeneo hatarishi na kutekeleza shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo salama,kutambua maeneo hatarishi na yenye viashiria vya kuathirika na maafa na kuandaa mipango ya kuzuia madadha na kukabiliana na maafa endapo yatatokea.
Pia Mhagama amesema madhara ya mvua kubwa yanaweza kujitokeza katika mikoa ambayo haihusiki na mvua hizo za Vuli na hali hiyo inatokana na mazingira ya kijiografia ya nchi ya Tanzania kuwa na mabonde, mabwawa na mito mikubwa ambayo inapokea maji mengi kutoka kwenye mikoa iliyopo katika uwanda wa milimani.
Hivyo, wananchi wote wanaoishi na kuendesha shughuli za kiuchumi maeneo ya uwanda wa chini na pembezoni mwa mabonde ya maji wanatahadharishwa kuchukua hatua ili kunusuru maisha na mali zao.
"Pamoja na madhara yanayoweza kujitokeza, naomba kutoa wito kwa umma kutumia mvua hizi vizuri ili ziwe na manufaa kupitia shughuli za uzalishaji mali kama kilimo, kuandaa mabwawa na malambo kwa ajili ya kuvuna maji, kupanda mazao yanayohitaji maji mengi kama vile mpunga, uzalishaji wa samaki na kuandaa na kuhifadhi malisho ya mifugo,"amesema Mhagama
Msimu wa Vuli ni mahususi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka unahusisha maeneo ya Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, kusini mwa mkoa wa Simiyu, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia) na Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro.
No comments:
Post a Comment