TANI 148,000 ZA ASALI KUUZWA NJE YA TANZANIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, August 5, 2023

TANI 148,000 ZA ASALI KUUZWA NJE YA TANZANIA


Na shua Ndereka

Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa amewataka wafugaji wa nyuki kuzalisha asali kwa wingi kwani Serikali imepanga kuuza nje ya nchi mwaka huu tani 148,000.


Amebainisha hayo Agosti 04, 2023 mara baada ya kutembelea banda la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika Uwanja vya Mwl. Julius Kambarage Nyerere Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.


Aidha Mchengerwa amesema kwa sasa asali inayouzwa ni asilimia 5 hivyo Serikali kupitia Wizara hiyo, imepanga kutoa elimu kwa wafugaji wa nyuki ili kuongeza kiwango cha uzalishaji na kufikia zaidi ya asilimia 50% ya asali inayouzwa nje ya nchi.


...tunauza asali nje ya nchi kwa 5% ambapo mpango wetu wa Wizara ni kuuza tani 148,000 za asali kwa mwaka huu, maana yake ni kwamba tuzalishe tani 148,000 tuongeze uzalishaji kutoka 5% ikibidi tufikie hadi 50%, hivyo tunategemea tuzalishe asali ambayo itakuwa na viwango na tutakayoipigia debe mataifa mengi yapo tayari kununua asali kutoka Tanzania, mataifa ya Waarabu, Ulaya, Amerika na maeneo mengine...” amesema Waziri Mchengerwa.


Waziri Mchengerwa amepongeza kazi inayofanywa na wakulima wadogo nchini, huku akifungua milango ya ushirikiano baina ya Taasisi ya MVIWATA na wizara ya Maliasili na Utalii ili kuboresha vikundi vya kuzalisha Asali pamoja na kufanya kazi kwa bidii.


Naye Mkuu wa Programu kutoka MVIWATA, Theodora Pius amesema wakulima wadogo wamekuwa na ubunifu mkubwa katika Sekta ya Kilimo kupitia mazao mbalimbali nchini.


“Wakulima wadogo wanao uwezo wa kulisha dunia kwa namna tofauti tofauti, tukiacha kwamba wanazalisha mazao lakini vipo viburudisho ambavyo wanatengeneza wakulima kutoka Njombe ikiwemo wine ya nyanya na zinginezo…”Amesema Theodora.


Katika hatua nyingine wakati akitoa shukrani kwa Waziri huyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima ameahidi kuandaa mazingira mazuri ya kuhifadhia wanyama ambao wamekuwa sehemu ya kivutio kikubwa cha maonesho hayo.


“..tutaweka utaratibu ili maonesho haya yasiishie kipindi cha Nanenane pekee, hivyo tutapanga nanenane kuwa na kivutio…”


Waziri Mchengerwa ametembelea mabanda mbalimbali yaliyopo katika maonesho ya nanenane ili kuona teknolojia mbalimbali na bidhaa zinazozalishwa nchini kupitia Kilimo, ufugaji na Uvuvi.

No comments:

Post a Comment