# Kwasasa sekta inahamia katika Madini Mkakati
#Tafiti zinaonesha uwepo wa Madini Mkakati kwa wingi
Wadau wa sekta ya Madini nchini watakiwa kugeukia fursa zilizopo katika Madini Mkakati na Madini adimu hii ni kutokana kuwa tafiti zinaonesha Tanzania ina hazina kubwa ya madini hayo.
Rai hiyo imetolewa leo Septemba 30 , 2023 na Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman wakati akifunga Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita yaliyoanza Septemba 20- 30, 2023.
Mhe. Suleiman amepongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kupiga hatua kubwa ya maendeleo kwenye madini ya dhahabu kuanzia hatua ya uchimbaji mpaka usafishaji ambapo kwasasa yameleta tija kibiashara kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
"Kama mnavyofanya katika madini ya dhahabu sasa mnaweza kuangalia upande mwingine wa madini Mkakati na Madini adimu ambayo yana thamani kubwa katika masoko" amesema Suleiman
Akitolea mfano baadhi ya Madini Mkakati kama vile Madini ya Titanium, Nikeli na Graphite , Mhe. Suleiman amewata wadau wa sekta ya madini kuanza kufikiria uwekezaji na Uthaminishaji katika Madini Mkakati na Madini adimu kwasababu tafiti zinaonesha kuwepo kwa wingi madini hayo ambayo yanahitajika kwa wingi.
"Niwaombe wadau wa madini kwa vile huku katika dhahabu ni safi sasa muanze kufikiria pia katika madini Mkakati" ,amesema Mhe. Suleiman
Kwa Upande wake , Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigella amesema hivi sasa Geita imepanga kutoa leseni 2,411 za uchimbaji madini ikiwa ni mpango wa kuwawezesha wachimbaji wadogo kuingia katika uchimbaji wenye uhakika.
Akielezea kuhusu mchango wa mkoa wa Geita katika pato la Taifa Shigella amesema kuanzia mwaka 2012 mkoa umekuwa ukichangia asilimia 5 katika pato la taifa na kushika nafasi ya saba.
Shigella ameongeza kuwa Mkoa wa Geita kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lina mpango wa kuwawezesha wachimbaji wadogo kutumia Teknolojia ya kisasa katika uchenjuaji badala ya Zebaki ambayo inatoa asilimia 25 na kupoteza asilimia 75 ya madini.
Naye , Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema Wizara ya Madini kupitia VISION 2030: Madini ni Maisha na Utajiri, inaendelea kuboresha sekta ya madini kwa kufanya utafiti wa kina wa jiosayansi kwa nchi nzima ifikapo 2030 lengo ni kuongeza wigo wa taarifa za uwepo wa madini.
Akifafanua kuhusu mchango wa sekta ya Madini Waziri Mavunde amesema kuwa kwa mwaka 2022 na 2023 sekta imeweza kuchangia asilimia 56 ya fedha za kigeni na asilimia 15 katika kodi za ndani.
Akielezea kuhusu mitambo ya uchorongaji Mhe. Mavunde, amesema tayari Serikali inatambua mchango wa wachimbaji wadogo hivyo imeagiza mitambo mitano ya uchorongaji ambayo itazinduliwa Oktoba 21, 2023 na Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Hassan.
Maonesho haya yamefungwa na kuambatana na Tuzo mbalimbali kwa Washiriki ambapo Wizara ya Madini kupitia Taasisi yake ya GST imepata tuzo ya Taasisi ya Umma Wezeshi na STAMICO imepata cheti cha pongezi na tuzo ya Utendaji Bora.
No comments:
Post a Comment