Na Mwandishi wetu- Lindi
Kamati za maafa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi zimekumbushwa kutoa elimu kwa jamii katika maeneo yao kuhusu namna ya kujiandaa na kukabiliana na maafa pamoja na kurejesha hali pindi majanga yanapotokea.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuzijengea uwezo kamati za maafa katika Manispaa hiyo kuhusu Upunguzaji wa madhara ya maafa katika jamii yaliyofanyika Ukumbi wa mikutano wa DDC mkoani Lindi .
Mkuu wa Wilaya hiyo amesema mafunzo hayo yanafanyika wakati muafaka ikiwa ni mwendelezo wa mikakati ambayo imekuwa ikifanywa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu katika kupunguza madhara ya maafa kwa kuhakikisha huduma za dharura zinatolewa kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuokoa watu na mali na kuwahimiza wadau wa kamati hizo kufahamiana ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
“Ni vyema wajumbe wa kamati mfahamiane ili ujue mdau gani unaweza kufanya naye kazi kwahiyo kupitia mafunzo haya kila mmoja afahamu ni mdau gani anapaswa kuwasiliana naye ili kutoa msaada kulingana na maafa yaliyotokea na kuokoa maisha ya watu na mali zao,”Amesema Mhe. Ndemanga.
Aidha Mkuu wa Wilaya hiyo amewasisitiza wajumbe wa kamati hiyo kutosubiri mpaka maafa yatokee badala yake wanatakiwa waijue historia ya eneo husika hatua itakayorahisisha kujipanga kwaajili ya maafa yatakayoweza kutokea na kutoa msaada kwa wakati.
“Niwaombe wajumbe wa kamati hizi tufuatilie na kusikiliza kwa karibu utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa sababu tutafahamu mambo gani tuwaambie wananchi wetu, tahadhari gani wachukue kabla ya maafa kutokea na hata yakitokeza wajue nini wanatakiwa kufanya,”Amesisitiza.
Akiwasilisha Mfumo wa Usimamizi wa Maafa nchini wakati wa semina hiyo Mratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Dorothy Pantaleo ameeleza baadhi ya sababu zinazosababisha kutokea kwa maafa akisema ni pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa, migogoro ya kisiasa, ukame, wadudu waharibifu na makazi kujengwa katika maeneo hatarishi.
“Maafa yanaweza kutokea kutokana na nguvu za asili au shughuli za kibinadamu ambapo wakati mwingine husababisha matetemeko ya ardhi, vimbunga, mafuriko, Volkano, umasikini na matatizo ya kijamii kwahiyo uwepo wenu kama kamati mnapaswa kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu namna ya kujiandaa, kujikinga na kukabiliana na maafa katika maeneo yenu,”Ameeleza Mratibu huyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Taasisi na Matawi kutoka Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS) Bw. Reginald Mhango amebainisha kuwa REDCROSS ina majukumu mengi yakiwemo kutoa huduma ya kwanza kwa watu walioathirika na kusaidia kurejesha hali baada ya maafa kutokea.
Nao baadhi ya wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi wakitoa maoni yao wamepongeza uundwaji wa kamati hizo kuanzia ngazi za Kijiji, Kata, Mtaa, Halmashauri, Wilaya, Mkoa na Kitaifa ambazo zitasaidia kuwa nampango kazi utakawezesha kukabiliana na maafa hatimaye kupunguza madhara yake kwa wananchi.
Akitoa maoni yake Mkazi wa Mtaa wa Mtanda katika Halmashauri hiyo Bw. Abdallah Madebe amesema kuundwa kwa kamati kutawezesha kufanyika kwa utafiti wa vyanzo vya maafa hatua itakayowezesha kufahamu hatua za kuchukua kujikinga, kujiandaa na kukabiliana na maafa.
Aidha Mkazi wa Mtaa wa Likotwa Bi.Faraja Mwingira ameeleza kuwa kila mmoja katika nafasi yake ana wajibu wa kufanya ili kukabiliana na maafa huku akisisitiza wananchi kuacha kupuuza utabiri wa hali ya hewa, tahadhari inayotolewa na wataalam na kufuatilia yombo vya habari ambapo elimu ya maafa hutolewa ili wapate uelewa wa kutosha .
No comments:
Post a Comment