![]() |
Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Morogoro Neema Haule, akizungumza leo Oktoba 10,2023 Mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo kuhusu Kanuni za ulinzi kwa watoa taarifa na mashahidi kwa waandishi wa habari. |
Na Okuly Julius - Morogoro
Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Morogoro Neema Haule,ametoa wito kwa waandishi wa habari nchini kuwa mabalozi na kuihabarisha umma kuhusu taratibu za Ulinzi kwa watoa taarifa na Mashahidi.
Haule ametoa wito huo leo Oktoba 10,2023 Mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo kuhusu Kanuni za ulinzi kwa watoa taarifa na mashahidi kwa waandishi wa habari.
"Waandishi wa habari ni daraja muhimu sana kwa kuifikia jamii hivyo kupitia mafunzo haya yanayotolewa kwenu yatawasaidia kuwa mabalozi na kuihabarisha umma kuhudu taratibu za Ulinzi kwa watoa taarifa na Mashahidi,"amesema Haule
Amesema kuwa Waandishi wa habari watapata fursa ya kuelimishwa kuhusu Sheria ya Ulinzi kwa Watoa Taarifa na Mashahidi Sura ya 446 na kanuni za Ulinzi kwa Watoa Taarifa na Mashahidi, kanuni zilizotolewa kupitia Tangazo la Serikali Namba 59 la tarehe 10 Februari, 2023 ili elimu hiyo waweze kuifikisha kwa jamii.
Haule ameongeza kuwa kutokana na uwepo wa Sheria na Kanuni hizo wananchi hawatakiwi kuwa na woga kujitokeza kutoa taarifa za uhalifu na matendo ya aina zote yanayofanywa kinyume cha Sheria kwani taarifa hizo zitakuwa siri na zitafanyiwa kazi bila ya kuwataja watoa taarifa.
Pia amewatoa hofu Mashahidi pindi wanapotakiwa kufika mahakamani kutoa ushahidi wasiogope kwani kanuni hizo zitawalinda dhidi ya Changamoto zote za kiusalama.
"Mkumbuke kuwa wanancji wanavyotoa taarifa hizo zitafanikisha kuokoa mali za umma ,kupatikana kwa wahalifu na kulinda Mazingira na maisha ya binadamu kutokana na uhalifu uliopangwa kufanyika , wamewekewa utaratibu wa kupatiwa motisha ikiwa ni pamoja na kuwafidia wale ambao wataathirika kutokana na taarifa wanazozitoa,"amesema Haule
Hivyo kuwataka wananchi Kushiriki katika mapambano dhidi ya uhalifu kwa kufika katika vyombo vya sheria na kutoa taarifa za uhalifu ili kutunza amani ,usalama na utulivu ambayo ni sharti muhimu la kutengeneza Mazingira wezeshi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Katiba kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Burton Mwasomola amesema lengo la Sheria na Kanuni hizo ni kufichua maovu katika jamii, makossa ya kiuhalifu ikiwemo ukiukwaji wa maadili kwa watumishi wa umma.
“Lengo ni kuhakikisha mashahidi wanalindwa kwa mujibu wa Sheria. Wote tuliowaita hapa majina yenu ni makubwa, nyinyi ni waandishi wa habari wanufaika wa mwanzo kabisa kwa sababu Sheria hii na kanuni hizi ni mpya kabisa. Tumewaita ili mkatusaidie kuielimisha jamii”,amesema Mwasomola.
Kwa upande wake, Mratibu Msaidizi, Ufuatiliaji na Tathmini Programu ya BSAAT, Ofisi ya Rais, Ikulu, Bw. Josiah Mathania amesema mafunzo hayo yanalenga kuwaelisha waandishi kuhusu sharia na kanuni ili kuwalinda watoa taarifa na mashahidi.
“Tunaamini nyinyi waandishi wa habari waandamizi mtasaidia kuelimisha wananchi kuhusu kutoa taarifa. Sasa wananchi wataweza kutoa taarifa bila uoga na taarifa zitaongezeka. Hizi taarifa sasa zitatoka bila hofu kwa wananchi ambao awali walikuwa wanapata hofu kutoa taarifa”,amesema.
Akielezea kuhusu Programu ya Building Sustainable Ant Corruption Action in Tanzania (BSAAT), amesema ni Programu ya kujenga mfumo endelevu wa kupambana na rushwa nchini ambapo lengo kuu ni kuisaidia serikali ya Tanzania katika juhudi zake za kupambana na rushwa kwa kuziwezesha Taasisi 10 zinazolenga kupambana na rushwa nchini.
Amezitaja taasisi hizo kuwa ni TAKUKURU,Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Sekretariati ya Maadili ya viongozi,Ofisi ya Msajili wa Makampuni,Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu, Mahakama ya Tanzania, Idara ya Utawala Bora na Maboresho, Ikulu.
Ameongeza kuwa Programu hiyo inaratibiwa na Ofisi ya Rais, Ikulu ikipata ufadhili kutoka Serikali ya Uingereza na Umoja wa nchi za ulaya (EU) ambapo kila mwaka kiasi cha takribani Shilingi Bilioni 6 kwa mwaka zinatolewa kwa Taasisi hizo 10.
“Programu ya BSAAT inapimwa kwa viashiria vikuu vitatu ambavyo ni kuongeza taarifa shuku za rushwa, kupunguza muda wa kesi mahakamani na kurejesha/kutaifisha mali zilizopatikana kwa njia ya rushwa”,ameeleza.
Ameongeza kuwa, Programu ya BSAAT ilifadhili Uandaaji wa Kanuni za Ulinzi kwa Watoa Taarifa na Mashahidi pamoja na mafunzo kwa waandishi waandamizi wa vyombo vya habari.
“Programu inaamini kuwa baada ya mafunzo haya, wananchi watapata uelewa wa kutosha kuhusu sheria na kanuni hizi kupitia vyombo vyenu vya habari, na hivyo kupelekea kufanikisha kiashiria kikuu cha kwanza cha program ya BSAAT cha kuongeza taarifa shuku za rushwa/uhalifu”, amesema Mathania .
Ikumbukwe kuwa Mwaka ,2015 Serikali kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipitisha Sheria ya Ulinzi wa Watoa Taarifa na Mashahidi ya Mwaka ,2015 (The Whistleblower and Witness Protection Act,2015) ikiwa na lengo la Kuimarisha utawala bora na mapambano dhidi ya uhalifu nchini kwa kuanzisha taratibu za kuwatambua na kuwalinda watoa taarifa na mashahidi.
No comments:
Post a Comment