DKT. MOLLEL: MAFANIKIO KATIKA SEKTA YA AFYA YANATOKANA NA UONGOZI BORA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, November 17, 2023

DKT. MOLLEL: MAFANIKIO KATIKA SEKTA YA AFYA YANATOKANA NA UONGOZI BORA


Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka waganga wakuu wa Hospitali za Rufaa za Mikoa na Wilaya kuboresha utoaji wa huduma katika hospitali zao na kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwakua Serikali haitamvumilia kiongozi yoyote anayekwamisha juhudi za uboreshaji wa huduma katika sekta ya afya nchini.

Dkt. Molel ametoa kauli hiyo leo alipofanya ziara katika Hoaspitali ya Taifa Muhimbili kuangalia hali ya utoaji huduma na kufanya mazungumzo na Wakuu wa Taasisi za Afya ikiwemo MNH, JKCI, MOI , MSD, NHIF,TMDA ,Mganga Mkuu wa mkoa pamoja na Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za mkoa wa Dar es saalam .

Akizungumza katika kikao hicho , Naibu Waziri wa Afya ameeleza kuwa mafanikio katika uboreshaji wa huduma sio uwekezaji wa vifaa tiba na rasilimali watu pekee bali ni pamoja na kuwepo kwa uongozi bora na kila mmoja kutimiza wajibu wake.

‘’Mh. Rais wa Awamu ya Sita Dkt.Samia Suluhu Hassan ameshamaliza kazi yake kwa kuwekeza Trilioni 6.7 katika miundombinu, taaluma, teknolojia tiba na rasilimali watu sasa ni wakati wa kila kiongozi kutekeleza majukumu yake kwakua sera ya Wizara ya Afya kwasasa ni kuhakikisha Hospitali za Serikali zinatoa huduma bora zinazokidhi viwango’’ amesema Dkt. Mollel

‘’Mh. Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ameniagiza kutembelea hospitali zote nchini kuangalia suala la ubora katika utoaji huduma na kufanya marekebisho katika maeneo ambayo hayafanyi vizuri, kiongozi kama hutekelezi majukumu yako inavyotakiwa unapaswa kujitafakari , hata hivyo napenda kuzipongeza Taasisi za MNH, MOI na JKCI kwa kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya afya ‘’amesisitiza Dkt. Mollel

Aidha Naibu Waziri wa Afya ameelezea kutoridhishwa na utendaji kazi wa mabaraza ya kitaaluma katika sekta ya afya nchini ambapo ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wajibu wao kwa kufuata miongozo ya taaluma zao kama inavyoelekeza.

Wakati huohuo Dkt. Mollel amesema Wizara ya Afya imedhamiria kuhakikisha kuwa mifumo ya TEHAMA katika hospitali kuanzia ngazi ya zahanati hadi taifa inasomana ili kumpunguzia muda mgonjwa wa kusubiri kupata matibabu kwa kurudia kufanya kipimo isipokua pale inapolazimu kurudia kufanya kipimo husika.


Awali akiwakaribisha katika kikao hicho , Mkurugenzi Mtendaji wa Hopsitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema MNH kama Hospitali ya Taifa inaendelea kujikita zaidi katika kutoa huduma za kibobezi ambazo hazipatikani katika Hospitali za Rufaa za Mkoa ili kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii tiba.


No comments:

Post a Comment