Na WMJJWM Arusha
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Seif Shekalaghe amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwekeza juhudi na ubunifu wa kugusa na kubadili fikra za watu ili kusaidia Taifa .
Dkt. Shekalaghe ameyasema hayo katika siku ya pili ya Kongamano la Maafisa Maendeleo ya Jamii linaloendelea Mkoani Arusha Novemba 21, 2023.
Amesema kuna umuhimu mkubwa wa Maafisa Maendeleo ya Jamii kujitoa kwa moyo bila kusukumwa katika utekelezaji wa majukumu yao na kutowekeza maslahi mbele.
“Inabidi kugusa mioyo na fikra za watu ili waweze kuona tunayowaelekeza yana tija katika maisha yao na si kuishia kujulikana tu kwa nafasi zetu. Tujikite na tuwekeze kwenye kupambana kutoa huduma rasilimali zitatufata” amesema Dkt. Shekalaghe.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Patrick Golwike amewakumbusha Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwafikia Wananchi kuanzia ngazi za kata ili kutatua changamoto zilizopo.
“Ukaribu baina ya Maafisa Maendeleo ya Jamii na Wananchi utarahisisha kazi na kutuwezesha kutekeleza majukumu yetu bila ugumu wowote kutoka kwa wananchi kwani ugumu huja pale ambapo walengwa wanakua hawaelewi manufaa ya uwepo wa Maafisa Maendeleo ya Jamii” amesema Golwike
Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda ameahidi kushirikiana hatua kwa hatua kuhakikisha kwamba maendeleo yaliyodhamiriwa na Serikali ya awamu ya sita yanafikiwa.
No comments:
Post a Comment