Na Okuly Julius - Dodoma
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph ametoa wito kwa wananchi kutokubali kushawishiwa, kutoa au kupokea Rushwa kwa kupita njia zisizo halali kupata huduma kutoka katika Mamlaka hiyo kwani huduma zote zinapatikana bure.
Amewataka pia wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona kuna changamoto katika utoaji wa Huduma kwenye Mamlaka hiyo na kama kutakuwepo na dalili ya kuombwa, kupokea au kutoa Rushwa.
Mhandisi Aron Joseph ametoa wito huo leo Disemba 3,2023 Jijini Dodoma baada ya kushiriki Mbio za "SEPESHA RUSHWA MARATHON" zilizoandaliwa na kuratibiwa na vijana waliokuwa wanachama wa Klabu za Wapinga Rushwa shuleni na vyuoni ambao baada ya kumaliza masomo, wakaanzisha Asasi ya Kiraia inayoitwa Anti – Corruption Voices Foundation (ACVF).
"Nimeshiriki katika Mbio hizi za "SEPESHA RUSHWA" nikiwa mdau, mtumishi umma na kiongozi wa Taasisi ambayo inawezekana kwa namna moja au nyingine ikajikuta inaingia kwenye mitego ya kupokea au kutoa Rushwa,hivyo sisi kama wadau wakubwa tunapiga vita utoaji au upokeaji wa Rushwa,"amesema Mhandisi Aron.
Amesema kupitia Kampeni za kupinga na kupambana Rushwa, DUWASA itaendelea kushiriki ili kuhakikisha wanapambana na Rushwa kivitendo katika utoaji wa huduma zake.
Pia ametumia Jukwaa hilo kutoa taarifa ya Maendeleo ya Mradi wa maji Nzuguni, ambapo amesema mpaka sasa mradi huo umefikia asilimia 96 na baadhi ya maeneo ya Nzuguni na Ilazo wameshaanza kupata huduma ya majisafi na mradi utakapokamilika kwa asilimia 100 maeneo ya Kisasa nyumba 300, Mwangaza, Swaswa,Ilazo na Nzuguni yote watapata huduma ya majisafi kwa uhakika.
No comments:
Post a Comment