![]() |
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Marry Makondo akizungumza Leo Disemba 4,2023 jijini Dodoma wakati wa Jukwaa la Kitaifa la Wadau wa Juhudi Dhidi ya Rushwa |

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais , Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.George Simbachawene amesema tafiti mbalimbali zilizofanyika ikiwemo ya Hali za Utawala Bora nchini zimebaini kuwa Rushwa ni moja ya changamoto ya ufikiwaji wa lengo la serikali la ustawi wa wananchi.
Akifungua Jukwaa la Kitaifa la Wadau wa Juhudi Dhidi ya Rushwa Disemba 4,2023 jijini Dodoma Mhe.Simbachawene amesema kuwa serikali haitaacha kukabiliana na adui Rushwa kwa njia za kuzuia na inapobidi kupambana nayo.
“Moja ya njia za kuzuia rushwa ni kama hii ya kujadili pamoja mbinu za kuboresha zaidi usimamizi wa miradi ya maendeleo ,hivyo ni matarajio ya Serikali kuwa wadau wa sekta zote kwa umoja wetu tutaitendea haki mada hii na hivyo kuweza kutoka na maazimio yatakayosaidia katika juhudi za kuzuia rushwa badala ya kusubiri na kupambana wakati tumeshapoteza rasilimali nyingi,” amesema Simbachawene
Mhe.Simbachawene amesema kuwa serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt.Samia imekuwa ikihamasisha zaidi kuzuia Rushwa na sio kupambana kwani inatambua vyema suala la kupambana na rushwa mara nyingi hakujawahi kurudisha rasilimali nyingi ambazo zimekuwa zikipotea kutokana na vitendo vya rushwa.
“ni vyema tutembee na Kaulimbiu ya TAKUKURU inayosema ‘Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu ;Tutimize Wajibu Wetu’ hivyo kila mmoja akumbuke anawajibu wa kuhakikisha fedha ya umma haipotei kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo,”amesisitiza Simbachawene
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Marry Makondo amesema kuwa Jukwaa la Kitaifa la Wadau wa Juhudi Dhidi ya Rushwa linatarajiwa kuwa na majadiliano yatakayochangia kuimarisha uzingatiaji wa maadili na haki za binadamu kwa kupinga rushwa Serikalini pamoja na sekta binafsi.
Amesema kutakuwa na wiki ya huduma kwa jamii kwenye viwanja vya Nyerere Square ambapo wadau wa Serikali na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayojihusisha na masuala ya maadili na haki za binadamu watatoa huduma mbalimbali kuanzia tarehe 5 hadi 10 Desemba, ambapo tarehe 10 Desemba itakuwa Siku ya Kilele.
Vilevile, kutakuwa na utoaji wa elimu kupitia vyombo mbalimbali vya habari ili umma ipate uelewa juu ya umuhimu wa kuizingatia maadili, kutokujihusisha na rushwa na kuzingatia haki za binadamu.
No comments:
Post a Comment