MAMBO YOTE YANAYOHUSU UPATIKANAJI WA MAJI UDOM CHINI YA DUWASA- MHE. AWESO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, January 23, 2024

MAMBO YOTE YANAYOHUSU UPATIKANAJI WA MAJI UDOM CHINI YA DUWASA- MHE. AWESO


Na Carlos Claudio, Dodoma 

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso ameipa DUWASA usimamizi wa upatikanaji wa maji katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) alipofanya ziara na kufuatilia hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi katika chuo hicho chenye wanachuo wapatao elfu 35.

Mhe. Aweso ameyasema hayo leo Januari 23,2024 alipotembelea na kukagua hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi mara baada ya kikao kifupi katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dodoma kabla ya kuanza ziara hiyo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Amesema UDOM ni sehemu muhimu na wanafanya kazi nzuri ikiwemo mchango mkubwa katika taifa kwani wahandisi na viongozi wote wametokana na elimu hivyo ni eneo muhimu na hatokuwa kikwazo kwasababu amepewa dhamana ya Wizara ya Maji na atahakikisha UDOM inapata maji safi na salama.


“Kuna kiasi cha shilingi bilioni 1 ambacho tumepewa lakini nimefwatilia menejimenti yake nadhani kunachangamoto kwenye swala la uratibu kwamfano nikiuliza hapa wanaosimamia eneo la UDOM kwenye upatikanaji wa maji ni nani majibu tutaambiwa ni DUWASA lakini fedha zimepelekwa RUWASA sehemu ambapo hawahusiki katika eneo la usimamizi kwa hiyo uwajibikaji lazima tumpe msimamizi maalum katika hili eneo yeye ndio atakuwa kiherehere katika kuhakikisha watu hawa wanapata huduma ya maji”.

“Baada ya kupata ile taarifa binafsi sikuridhika na utendaji na hata naibu katibu mkuu nadhani umeona kwaio tutaweka nguvu na tutaongeza usimamizi kuhakikisha hili jambo tunaweka sawa, kwaio mambo yote yanayohusiana na upatikanaji wa maji UDOM yatakuwa chini ya DUWASA kwasababu mimi ninachokijua mamlaka ili iende maana yake kuna watu ambao wanaendesha mamlaka na hawa ndio watu wa kwanza kuangalia,”amesema mhe. Aweso.

Mhe Aweso ameongeza kwa kusema mahitaji ya jiji la Dodoma yameongezeka kwani uwezo wa mamlaka ya maji ilikuwa na uwezo wa kuzalisha maji zaidi ya lita milioni 60 na mahitaji ya jiji zima ilikuwa lita milioni 40 lakini sasaivi mahitaji yameongezeka hadi kufikia lita milioni 120.


Kwa upande wa makamu mkuu wa chuo Profesa Lughano Kusiluka amewasilisha taarifa fupi kuhusu hali ya maji katika Chuo Kikuu Cha Dodoma na amesema changamoto ya maji ni kubwa kwani idadi ya wanafunzi wanaotumia maji inaongezeka kwa sasahivi kuna takribani idadi ya wanafunzi elfu 35 ambao wanaendelea na usajili.

“Mwaka jana tulifanya utafiti mdogo wa idadi ya watu ambao ni watumiaji wa maji hapa Chuo Kikuu Cha Dodoma pamoja na kiwango cha maji ambacho tunahitaji ilionekana kama watumiaji, wakazi na wale wanaopita wanaweza kufika kama elfu 39 na kwasababu hiyo kiwango cha maji ambacho wenzetu wa DUWASA uwezo ilikuwa kutupa takribani lita milioni 1,172,000 kwa siku lakini mahitaji halisi kwa muujibu wa utafiti huo mdogo ni kwamba tunahitaji maji takribani lita 2,296,000 na kwa hiyo kwa kiwango ambacho tunachokipata sasahivi ni wastani wa asilimia 51% ya maji ambayo tunahitaji.”amesema profesa Kusiluka.

Mhe. Aweso katika ziara hiyo ameambatana na Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa na Wilaya ya Dodoma, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri, Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DUWASA), wataalamu kutoka Wizara ya Maji, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Clement Kivegalo.

No comments:

Post a Comment