Na, Roda Simba , OKULY BLOG , Dodoma
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe, amezitaka Taaasisi mbili za Wakala wa usajili wa biashara na Leseni (BRELA) pamoja na Tume ya Ushindani (FCC) kutimiza wajibu wao wa kujenga uchumi imara,na kuzingatia maelekezo ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kuziwezesha sekta binafsi zikue na kuongeza pato la Taifa.
Kadhalika Kigahe ameitaka BRELA iendelee kutoa elimu zaidi kwa wananchi ili warasimishe biashara zao huku akisema kwa kufanya hivyo itawasaidia wananchi hasa wajasiriamali wadogo ambao wanachangamoto ya kupata mitaji.
Kigahe ameyasema hayo leo Februari 11 2024 jijini Dodoma mara baada ya kukamilika semina ya wabunge wa kamati ya kudumu ya bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambayo ilienda sambamba na kupokea taarifa ya taasisi hizo mbili, BRELA na FCC.
"Taasisi nyingi za fedha zinapenda zione wafanyabiashara wanaotambulika,sasa BRELA ndio wanakazi kubwa ya kuhakikisha kuwa wanawasaidia kuwatambua hawa wote ambao wanafanya shughuli mbalimbali iwe kwenye biashara au kuanzisha viwanda vidogo hata viwanda vikubwa,
"Lakini pia wafanyabiashara hawa wangependa kuona biashara zao zinashindana kwa haki ndio inakuja jambo la ushindani wa haki yani (Fair competition) sasa lazima wananchi wajue nini tumefanya ili kuhakikisha tunawalinda wafanyabiashara wawe na haki,wanaozalisha ndani,lakini pia hata wale wanaoingiza bidhaa kutoka nje ili wanapoingia kwenye soko la Tanzania wajue tuna taratibu na kanuni" amesema Kigahe
Ameongeza kuwa kwa sasa wanalenga kuhakikisha Tume ya Ushindani FCC ina saidia kudhibiti bidhaa feki na bandia ambazo bado zina changamoto.
Nae Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Deo Mwanyika ambae pia ni mbunge wa jimbo la Njombe amesema Taaasisi hizo mbili za BRELA na FCC ndio uhai wa mazingira ya biashara na amekiri wamepokea mabadiliko makubwa.
"Nyuma hali ilikuwa mbaya zamani kusajili kampuni au taasisi ilikua inachukua muda mrefu ila kwa sasa ni siku mbili ya tatu mtu ambae amekamilisha nyaraka zake zote anapokea cheti cha usajili wa kampuni yake na hili kama nchi niseme tumevuka na itaongeza kuleta wawekezaji zaidi"amesema Mwanyika
Amesema wao kama kamati wajibu wao ni kuweza kuelewa zaidi ili kutekeleza jukumu la kuisimamia serikali,hivyo amesema ni lazima wawe na ufahamu wa taasisi hizo mbili za FCC na BRELA namna zinavyofanya kazi na kujua changamoto zao.
"Katika baadhi ya mambo ambayo bunge liliambiwa na Rais Samia mara baada ya kuchukua nafasi ni pamoja na suala zima la kuweka mazingira rafiki ya biashara"amesema
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Godfrey Nyaisa amesema ni utaratibu wao wa kawaida kuwapatia mafunzo wabunge kwa kuwa wao ndio wawakilishi wa wananchi.
" lengo zima ni katika kufanya maboresho na kuwahudumia watanzania na sisi kama BRELA tumewaelezea wabunge tunaenda kupitia sheria za makampuni ambayo ya zamani tutapitia na kuweka sawa ili twende na wakati uliopo katika kuhudumia wafanyabiashara na biashara zao zikue badala ya kuweka sheria zenye makwazo"amesema Nyaisa
William Erio ni Mkurugenzi Mkuu wa FCC ambapo amesema wanapendekeza sheria ya ushindani ifanyiwe marekebisho ili iweze kufanya vizuri hasa katika kuidhinisha miungano ya makampuni na kusema kwamba sheria waliyonayo ni ya mwaka 2003 na kwa sasa ina miaka 21 ambapo mazingira ya ufanyaji biashara yalikua tofauti katika kipindi hicho.
"Tumetaka maboresho ya sheria yetu ambayo tunapendekeza ifanyiwe marekebisho ili iweze kufanya vizuri zaidi hasa katika kuidhinisha miungano ya makampuni"amesema Erio
No comments:
Post a Comment