SERIKALI KUWASHUGHULIKIA WANAOWADHALILISHA WAKOPAJI MITANDAONI KWA MIKOPO KAUSHA DAMU - OKULY BLOG

Breaking

Home Top Ad

TANGAZA NASI HAPA | PIGA 0785 364 965

Thursday, February 22, 2024

SERIKALI KUWASHUGHULIKIA WANAOWADHALILISHA WAKOPAJI MITANDAONI KWA MIKOPO KAUSHA DAMU

Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro akizungumza wakati wa Mafunzo ya Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri yaliyofanyika jijini Dodoma, Wizara ya Fedha katika ukumbi wa Kambarage.
Afisa Mkuu Mwandamizi, Idara ya Usimamizi wa Huduma ndogo za Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Deogratias Mnyamani, Akitoa mada kuhusu Kanuni za Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha za mwaka 2019 kwa Daraja la pili; wakati wa mafunzo kwa waratibu wa Biashara ya Huduma ndogo za Fedha na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, yaliyofanyika jijini Dodoma, Wizara ya Fedha katika ukumbi wa Kambarage.
Baadhi ya Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, wakifuatilia mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dodoma, Wizara ya Fedha katika Ukumbi wa Kambarage.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)

Na Eva Ngowi na Asia Singano

Serikali imetoa wito kwa watoa huduma za kifedha nchini kufuata sheria na taratibu za huduma za Fedha ikiwemo kupata leseni ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuhakikisha huduma hizo zinatolewa kwa ufanisi bila kuwaumiza na kuwadhalilisha wanufaika na hatimaye kukuza uchumi wa nchi.

Akizungumza wakati wa mafunzo kwa waratibu wa Biashara ya Huduma ndogo za Fedha na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, Afisa Mkuu Mwandamizi, Idara ya Usimamizi wa Huduma ndogo za Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Deogratias Mnyamani alisema kuwa, Benki Kuu chini ya Wizara ya Fedha na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa mikakati kupitia sheria ya huduma ndogo ya Fedha ya mwaka 2018, ili kukomesha udhalilishaji unaofanywa na baadhi ya watoa huduma ndogo za fedha kupitia mitandao ya simu.

Benki hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha imeona umuhimu wa kutoa elimu ya fedha nchi nzima ili kuwapa uelewa wananchi kuhusu namna bora ya kukopa fedha na kuweza kurejesha mkopo bila kudhalilishwa.

Bw. Mnyamani alisema mikopo inayotolewa kwa njia ya mitandao ya simu imekuwa changamoto kubwa hasa katika ukusanyaji wa madeni kutoka kwa wakopaji jambo linalopelekea watoa huduma hao kuvunja sheria ya usiri inayotakiwa katika kupata huduma ya fedha kwa kuwadhalilisha wakopaji hao kwa kutuma ujumbe mfupi kwa ndugu na jamaa waliochukua mikopo hiyo. 

‘’Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania tunahitaji kushirikisha, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Makampuni ya simu na Polisi ili kuona namna ambayo tunaweza kulitatua suala hili la udhalilishaji linalofanywa na watoa huduma za fedha kupitia mitandao ya simu’’ alisema Bw. Mnyamani.

Bw. Mnyamani aliongeza kuwa Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania hivi karibuni itaendesha kampeni kupitia vyombo vya habari na njia mbali mbali za kutoa elimu kwa umma ili kujenga uelewa kwa wananchi na watoa huduma ndogo za fedha kuhusu masuala muhimu ya kuzingatia katika utoaji na upatikanaji wa huduma ndogo za fedha nchini.

Awali, akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro alisema ni wajibu wa watoa huduma ya fedha kutoa elimu kwa wananchi wanaoomba mikopo ili kuwawezesha kutumia mikopo hiyo kuzalisha faida na kuweza kurejesha kwa wakati.

Bw. Kimaro alisisitiza kuwa ni lazima mkopaji apewe elimu ya kutosha ili apate uelewa kuhusu masharti yaliyoanishwa kwenye mkataba kwa kupewa nafasi ya kusoma na kuuelewa mkataba wa mkopo kabla ya kuchukua mkopo husika.  

"Ni lazima mkopaji apewe elimu ya kutosha ili apate uelewa, na apewe nafasi ya kusoma na kuelewa mkataba wa mkopo kabla ya kuchukua mkopo’’ alisema Bw. Kimaro.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha, kutoka Mkoa wa Ruvuma, Bernard Evarist Ndikaniki, alisema mafunzo waliyopata yataikomboa jamii dhidi ya watoa huduma wasiokuwa waaminifu na kuchangia maendeleo ya nchi.

Bw. Ndikaniki aliongeza kuwa mafunzo hayo hayataishia tu kutoa faida kwa washiriki, lakini pia yanaenda kugusa jamii na ngazi ya chini kabisa ya wananchi yakiwa na lengo la kufikisha elimu hiyo kwa jamii ambayo ndio walaji wa mwisho wa huduma ndogo za fedha.

Mafunzo ya Waratibu wa Biashara ya Huduma ndogo za fedha na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri hufanyika kila mwaka, lengo likiwa ni kuimarisha huduma jumuishi za kifedha ili kuleta ufanisi wa utoaji huduma kwenye Sekta ndogo ya fedha nchini kwa wananchi wenye kipato cha chini ili kuwakwamua kiuchumi.

No comments:

Post a Comment

HABARI KUU KWA SASA

MADIWANI MANISPAA YA TEMEKE WAMEUSHUKURU UONGOZI WA KITUO CHA UHUSIANO WA KIMATAIFA CHA DKT. SALIM AHMED SALIM KWA KUWAPATIA MAFUNZO

Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam   Naibu Meya wa Manispaa ya Temeke Mheshimiwa Arnold Emmanuel Peter ameushukuru Uongozi wa Kituo cha Uhusian...