
Na OKULY JULIUS, OKULY BLOG, DODOMA
TUME ya Utumishi wa Umma (TUU) imejipa siku 60 kufanya utafiti kuhusu utoro kazini, unaotajwa kuwa miongoni mwa changamoto tano zinazohitaji hatua za haraka katika utumishi wa umma, ili kubaini chanzo chake na kuishauri Serikali kuhusu namna bora ya kukabiliana na tatizo hilo.
Katibu Mkuu wa Tume hiyo, Nolasco Kipanda, amesema utafiti huo unalenga kubaini sababu zinazochangia utoro kazini na kutoa mapendekezo yatakayosaidia mamlaka husika kuchukua hatua stahiki za kudhibiti tatizo hilo.
Kipanda ametoa kauli hiyo Oktoba 22, 2026, wakati akielezea maazimio ya mkutano wa kwanza wa Tume kwa mwaka wa fedha 2026/27, uliofanyika kuanzia Septemba 21 hadi Oktoba 16, mwaka huu, katika ofisi za Tume zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.
Amesema utoro kazini ni miongoni mwa maeneo matano yaliyobainika kuwa na changamoto katika utumishi wa umma, huku mengine yakiwa ni kushindwa kutekeleza majukumu, wizi wa mali za umma, rushwa, kughushi vyeti na kutoa taarifa za uongo.
“Tume imechukua maeneo matano ambayo tunaona yana changamoto, na katika maeneo hayo, utoro kazini unaongoza. Tumekubaliana kufanya utafiti ili tuweze kuzishauri mamlaka husika,” amesema Kipanda.
Ameeleza kuwa utafiti huo utachukua siku 60 kuanzia Oktoba 22, 2026, ambapo matokeo yake yatasaidia kuandaa mapendekezo ya kukabiliana na utoro kazini na kuimarisha uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa umma.
Aidha, amesema Tume inalenga kupunguza malalamiko na rufaa zinazotokana na masuala ya kiutumishi, akibainisha kuwa hatua hiyo inahitaji waajiri na waajiriwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia utumishi wa umma.
Katika mkutano huo, Tume ilipokea rufaa na malalamiko 74, zikiwemo rufaa 57 na malalamiko 17, yaliyohusu masuala mbalimbali ya ajira na nidhamu kwa watumishi wa umma.
Masuala yaliyowasilishwa yalihusu kupinga kutenguliwa katika cheo, kutorudishwa kazini, kusitishiwa ajira, kuondolewa kwenye orodha ya mishahara na kutopandishwa cheo.
Kwa mujibu wa Kipanda, warufani 18 na mrufaniwa mmoja walifika mbele ya Tume kusikilizwa. Vilevile, mamlaka mbili za nidhamu ziliitwa na kufika mbele ya Tume kuhojiwa kuhusu ukiukwaji wa sheria katika kushughulikia mashauri ya watumishi walio chini yao.
Katika hatua nyingine, Tume ilifanya ziara katika taasisi 14 za Serikali zilizopo mkoani Dodoma kwa lengo la kutoa elimu kuhusu masuala ya utumishi wa umma na kuimarisha uelewa wa sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia sekta hiyo.
Kipanda amezitaka mamlaka za ajira na nidhamu kuzingatia sheria wakati wa kushughulikia malalamiko na mashauri ya kinidhamu ya watumishi wa umma, ili kuhakikisha maamuzi yanayofanywa yanazingatia haki.
Amesisitiza kuwa uwajibikaji na uzingatiaji wa sheria kwa waajiri na waajiriwa ni mambo muhimu katika kupunguza malalamiko na rufaa zinazowasilishwa mbele ya Tume, pamoja na kuimarisha ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.





No comments:
Post a Comment