TARURA YAFANYA TATHMINI YA UBORA WA BARABARA ZILIZOJENGWA KWA KUTUMIA MALIGHAFI ZA ENEO HUSIKA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, October 20, 2026

TARURA YAFANYA TATHMINI YA UBORA WA BARABARA ZILIZOJENGWA KWA KUTUMIA MALIGHAFI ZA ENEO HUSIKA


Na Mwandishi Wetu - Dodoma


Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Edward Amboka ameongoza kikao cha wataalamu wa Kitengo cha Tafiti na Udhibiti Ubora kilicholenga kujadili matokeo ya ufuatiliaji wa ubora na uimara wa barabara zilizojengwa kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika maeneo husika.

Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za mradi wa RISE jengo la PSSSF jijini Dodoma, kimejadili matokeo ya ufuatiliaji wa barabara ya Shewa yenye urefu wa kilomita 2 na barabara ya Mbalizi–Malowe–Songwe–Magereza yenye urefu wa kilomita 2 zilizojengwa kwa teknolojia ya mawe ambazo zipo jijini Mbeya.

Barabara hizo zimejengwa kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika maeneo husika na kukamilika mwaka 2024.

Ufuatiliaji huo ulifanyika katika kipindi cha miaka miwili ili kutathmini utendaji, uimara na uwezo wa barabara hizo kuhimili matumizi na hali mbalimbali za kimazingira hatua inayolenga kubaini ufanisi wa teknolojia hiyo ya ujenzi na uwezekano wa kuitumia katika maeneo mengine yenye malighafi zinazofaa.

Matokeo ya tathmini hiyo yanatarajiwa kusaidia TARURA kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi ya teknolojia hiyo katika ujenzi wa barabara nyingine, kuongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali zilizopo katika maeneo husika na kupunguza gharama za ujenzi bila kuathiri ubora wa miundombinu.

Ripoti ya utafiti huo imewasilishwa na Profesa Duwa Changula kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (Mbeya University of Science and Technology – MUST), ambaye aliongoza utafiti huo.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhandisi Amboka amewapongeza wataalamu na washiriki wa utafiti huo kwa kazi nzuri waliyoifanya huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya TARURA, taasisi za elimu ya juu na wataalamu mbalimbali katika kufanya tafiti zitakazochangia upatikanaji wa suluhisho bunifu na endelevu katika ujenzi wa barabara.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia utunzaji wa mazingira katika hatua zote za ujenzi wa barabara akieleza kuwa matumizi ya teknolojia na malighafi zinazopatikana katika maeneo husika yanapaswa kwenda sambamba na usimamizi mzuri wa mazingira ili kuhakikisha maendeleo endelevu ya miundombinu.

No comments:

Post a Comment