BURUHANI, AAHIDI KUIREJESHA JUMUIYA KATIKA MISINGI YA KUANZISHWA KWAKE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, October 20, 2026

BURUHANI, AAHIDI KUIREJESHA JUMUIYA KATIKA MISINGI YA KUANZISHWA KWAKE

 


Na Boniphace john Dododma.


Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Faris Buruhani, amepokewa leo Oktoba 19, 2026 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Dodoma, ikiwa ni siku nane tangu ateuliwe Oktoba 11, 2026.


Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Buruhani amesema yeye na viongozi wenzake wamekusudia kuhakikisha Jumuiya hiyo inarejea katika misingi ya kuanzishwa kwake.


Amesema miongoni mwa misingi hiyo ni kuwaunganisha vijana wote wa Tanzania bila kujali tofauti za dini, makabila, siasa au hali zao za maisha.



Buruhani amebainisha kuwa uongozi wake utaweka msisitizo katika kuwajenga vijana kisiasa na kiitikadi, kuwashirikisha kikamilifu katika shughuli za Chama na kuwaandaa kushika nafasi za uongozi ndani ya CCM na Taifa kwa ujumla.


Aidha, Katibu Mkuu huyo amesema UVCCM ya sasa inahitaji kizazi kipya cha vijana wenye ujasiri, nidhamu na uzalendo wa kweli kwa Taifa, ambao hawataogopa kusimamia na kutetea maslahi ya Taifa pale yanapokuwa hatarini.


"Vijana wa UVCCM wanapaswa kuwa na uwezo wa kushiriki mijadala mizito ya kitaifa, kuelewa kwa kina sera na itikadi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kutanguliza maslahi ya Chama na Taifa badala ya maslahi binafsi," amesema Buruhani.


Katika hafla hiyo, Buruhani pia amesisitiza umuhimu wa vijana kuwa na msimamo thabiti wa kukitanguliza Chama kabla ya watu binafsi, akieleza kuwa uongozi ni wa kupokezana na hakuna anayebaki kwenye nafasi milele.

Amesema Jumuiya inahitaji vijana ambao watakuwa tayari kusimamia maelekezo na maamuzi ya Chama wakati wote, bila kuyumbishwa na maslahi ya mtu mmoja au makundi ya kisiasa.


Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Dodoma, Abdulhabib Mwanyemba, amewataka vijana kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali ndani ya Jumuiya hiyo na Chama Chamapinduzi kiujumla ifikapo uchaguzi wa Chama Hivi karibuni.


Mwanyemba amesema vijana wasiwe na hofu ya kugombea akitolea mfano hata nafasi yake mwenyewe iko wazi kwa yeyote mwenye sifa na uwezo.


"Wagombee tu, wasiogope. Hata nafasi yangu waje wagombee. UVCCM ni ya vijana wote," amesema Mwanyemba.


Pia Mwanyemba amemuomba Katibu Mkuu huyo kuwa mtetezi wa vijana.


Amesema anatarajia uongozi mpya utasimamia haki, uwazi na kukataa vikali tuhuma na vitendo vya rushwa ndani ya Jumuiya ili kulinda hadhi na mustakabali wa vijana.

No comments:

Post a Comment