Na Boniphace John -Dodoma
Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) imetangaza kuwa ni wataalamu 4,449 pekee kati ya 22,269 waliosajiliwa ndio wanachama hai waliokidhi vigezo vya kitaaluma na wanaostahili kutekeleza majukumu ya ununuzi na ugavi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Oktoba 19, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Godfred Mbanyi, amesema hali hiyo imechochea Bodi kuandaa orodha rasmi ya majina ya wanachama hai wa kitaaluma itakayowekwa kwenye tovuti yake.
Amesema orodha hiyo itawawezesha waajiri wa sekta ya umma na binafsi kuhakiki uhalali wa wataalamu kabla ya kuwapa majukumu yanayohusiana na ununuzi na ugavi.
Mbanyi ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa shughuli za ununuzi na ugavi zinafanywa na wataalamu waliokidhi vigezo vinavyotakiwa kisheria.
Amesema PSPTB ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Fedha, iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya PSPTB, Sura ya 179 ya Sheria za Tanzania, ikiwa na jukumu la kusimamia na kudhibiti viwango vya kitaaluma, mwenendo na maadili katika taaluma ya mnyororo wa ugavi nchini.
Kwa mujibu wa Mbanyi, kwa mujibu wa Kifungu cha 7(g) cha Sheria ya PSPTB, Bodi imepewa mamlaka ya kusajili watu waliokidhi vigezo vya kitaaluma na kuwapa utambuzi wa kisheria wa kutekeleza majukumu ya kitaalamu katika fani hiyo.
Aidha, amesema Kanuni ya 38(1)(b) ya Kanuni za PSPTB za mwaka 2009 inaipa Bodi mamlaka ya kumfuta mtu kwenye usajili endapo atashindwa kulipa ada kwa kipindi kinachozidi miezi 24, hatua inayosisitiza umuhimu wa wataalamu kuzingatia masharti ya usajili na uanachama.
Mbanyi amesema orodha ya wanachama hai itawekwa kwenye tovuti ya PSPTB na itakuwa ikisasishwa kila wiki kwa kuongeza majina ya wataalamu watakaokuwa wamekidhi vigezo.
"Kwa mujibu wa sheria, orodha hii itakuwa nyenzo muhimu kwa waajiri na taasisi mbalimbali katika kuhakiki uhalali wa wataalamu wanaowaajiri," amesema Mbanyi.
Hivyo, ametoa wito kwa waajiri wote wa sekta ya umma na binafsi kuhakikisha kuwa shughuli za ununuzi na ugavi zinafanywa na wataalamu ambao majina yao yapo kwenye orodha rasmi ya wanachama hai iliyowekwa kwenye tovuti ya PSPTB.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa waajiri kuzingatia matakwa ya kisheria ili kuimarisha weledi, uwajibikaji na uzingatiaji wa maadili katika utekelezaji wa shughuli za ununuzi na ugavi nchini.



No comments:
Post a Comment