
Serikali kupitia Ofisi ya Raisi, Maendeleo ya Vijana imewatambua na kuwatunuku tuzo wadau wa mbolea vijana walioonesha ubunifu katika kukuza tasnia ya mbolea nchini na kuwezesha vijana wengi kujikwamua kiuchumi na kupunguza changamoto la ajira kwa vijana.
Hayo yamebainishwa tarehe 12 Oktoba, 2026 wakati wa hafla za kilele cha Kongamano la vijana lililofanyika katika ukumbi wa Nazareth Sumbawanga mkoani Rukwa kuelekea kilele cha mbio za Mwenge.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo ya wakala bora kijana wa usambazaji wa mbolea Oraph Stanley Mhema, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mhema Agrovert Limited ameeleza kuwa miaka kumi iliyopita alianza biashara yake ya mbolea kwa mtaji wa shilingi laki Sita (600,000) mpaka sasa ameweza kufikisha mtaji wa zaidi ya kiasi cha bilioni mia moja (100,000,000,000).
Mhema amesema kuwa hadi sasa amesajili mawakala vijana zaidi ya 300, huku akilenga kuongeza idadi hiyo hadi kufikia 600. Amesema mawakala hao watasaidia kusogeza pembejeo karibu na wakulima, kuwaondolea usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kuzifuata na hivyo kutekeleza azma ya Serikali ya kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo ndani ya umbali usiozidi kilomita tano (5).
Kwa upande wake Mbunifu wa Mfumo wa kidijitali wa pembejeo za ruzuku, Mahmoud Shoo ameeleza nia yake ya kuendelea kuongeza juhudi katika kujenga mifumo ya kidijitali ili kuweza kurahisisha upatikanaji wa takwimu na kuiwezesha serikali kuweka na kupima ufikiwaji wa malengo iliyojiwekea katika kuhudumia wananchi.
Naye David Denis Mbunifu na Mwanzilishi wa Kampuni ya Cuttoff Recycle Limited aliyetunukiwa tuzo ya kutambua mchango na ubunifu wa vijana katika uzalishaji wa mbolea amewataka vijana kutumia changamoto zilizopo katika maeneo yao na kutengeneza fursa ya kujipatia kipato na kukuza uchumi wao.
Amesema, aliona changamoto ya takataka ya nywele na kuamua kuzitafiti kuona ni namna gani zinaweza kutumika katika kukuza uchumi wake na ndipo akabaini ni chanzo kizuri cha kirutubisho cha nitrojen na kuamua kuzalisha mbolea kupitia nywele.
Kwa pamoja wabunifu hawa wameishukuru serikali na kuahidi kuendelea kuweka juhudi katika kazi zao na kuhakikisha wanachangia katika kutoa ajira kwa vijana ili kushiriki uchumi kupitia bunifu zao.





No comments:
Post a Comment