BASHUNGWA ATOA MASAA MATATU KUREJESHWA MAWASILIANO YA BARABARA YA MTWARA - MASASI ILIYOKATIKA. - OKULY BLOG

Breaking

Home Top Ad

TANGAZA NASI HAPA | PIGA 0785 364 965

Monday, March 4, 2024

BASHUNGWA ATOA MASAA MATATU KUREJESHWA MAWASILIANO YA BARABARA YA MTWARA - MASASI ILIYOKATIKA.


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameelekeza Wakala wa Barabara (TANROADS) kuhakikisha wanarejesha mawasiliano ya barabara iliyokatika eneo la Maili Mbili katika barabara ya Mtwara-Mingoyo-Masasi ndani ya masaa matatu mara baada ya Daraja kusombwa na maji katka eneo hilo.

Bashungwa ametoa agizo hilo tarehe 04 Machi, 2024 Wilayani Masasi akiwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Deo Ndejembi, alipofika hapo kujionea adha ya watumiaji wa barabara hiyo waliokwama tangu majira ya asubuhi kutokana na kukatika kwa miundombinu hiyo iliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha usiku wa jana.


“Nitoe pole kwa wananchi ambao mmepata changamoto kutokana na kukatika kwa mawasiliano ya barabara inayotoka mkoa wa Ruvuma kuelekea mkoa wa Mtwara na Lindi, Natoa saa tatu kwa TANROADS kuhakikisha inakamilisha kujenga barabara ya mbadala ili magari na wananchi waanze kupita", amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa ameeleza kuwa tayari Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa fedha za kumtafuta Mkandarasi atakayeijenga upya barabara hiyo ya Mtwara-Mingoyo-Masasi (km 200) kwa kiwango cha lami kwa kuwa barabara hiyo imekwisha muda wake na imechakaa.

“Wizara ya Ujenzi tumeshapokea maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan hadi kufikia Mwezi wa Sita Mkandarasi awe ameshapatikana na kuanza kazi ya kuijenga upya barabara hii”, amefafanua Bashungwa.

Naye, Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Deo Ndejembi ameeleza kuwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa kiasi cha Shilingi Bilioni 30 kwa ajili ya dharura za matengenezo ya barabara nchi nzima kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) na hivyo wamejipanga vyema kutatua changamoto zozote za mawasiliano ya barabara pindi zinapotokea.

Kwa upande wake Mbunge wa Masasi, Geofrey Mwambe, ameishukuru Serikali na timu nzima ya watalaam wa TANROADS kwa kuchukua hatua za haraka za kuhakikisha wanaanza kazi ya kurejesha mawasiliano ya barabara hiyo na miundombinu mingine ambayo imeathiriwa na mvua katika Wilaya ya Masasi.

No comments:

Post a Comment

HABARI KUU KWA SASA

HABARl ZILIZOPEWA UZITO WA JUU KATIKA MAGAZETI YA LEO MEI 6,2024