Na Okuly Julius-Dodoma
Amesema upatikanaji wa umeme umeongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2000 hadi 78 mwaka 2022. Vile vile, mtandao wa barabara za lami na zege mijini na vijijini umeongezeka kutoka KM 1,360 mwaka 1961 hadi KM 11,966 mwaka 2022.
Dkt. Jafo amesema hayo Machi 25, 2024 jijini Dodoma alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema Muungano huo umedumu kutokana na utashi wa dhati wa kisiasa waliokuwa nao waasisi wa muungano ambao uliwezesha vyama vya siasa vya TANU na ASP kuungana na kuunganishwa kwa vyama hivyo kumeongeza hali ya umoja na ushirikiano baina ya watu wa Tanganyika na Zanzibar.
“Utekelezaji wa mambo ya Muungano unazingatia Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yale mambo yasiyo ya Muungano yanazingatia sheria, mipango, sera, programu na mikakati ya maendeleo ambayo Serikali zote mbili zimejiwekea kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa Watanzania,”
Na kuongeza kuwa “Tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa vikao vya pamoja mwaka 2006 hadi sasa, kasi ya utatuzi wa changamoto imeongezeka ambapo hoja 22 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 25 zilizoibuliwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024 pekee, hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 18 zilizokuwepo kwa kipindi hicho,” amesema Dkt. Jafo
Pia Dkt. Jafo amesema katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2022, takribani shilingi bilioni 1.4 zimekuwa zikipelekwa Zanzibar kila mwaka na kuanzia mwaka 2023 shilingi bilioni 1.75 na kwa mwaka 2024 shilingi 2,034582,000 zimekuwa zikipelekwa Zanzibar kila mwaka na kufanya jumla fedha zilizopelekwa Zanzibar kwa kipindi hicho kuwa shilingi 20,874,314,940.00.00.
Dkt. Jafo ametoa rai kwa wananchi wote wa Tanzania kuendelea kuuenzi na kuutunza muungano ambao ni adhimu iliyodumu kwa miaka 60 na kuwa muungano wa kipekee barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Katika hatua nyingine amesema, katika utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, jumla ya Sheria Ndogo 326 zimeandaliwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Mikoa ya Dodoma (15), Kilimanjaro (7), Mbeya (57), Mtwara (69), Morogoro (53), Pwani (59) na Ruvuma (66).
Pia, mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 3.3 ulitekeleza mafunzo ya mabadiliko ya tabianchi kwa wataalam zaidi ya (80) wa Halmashauri za wilaya ya Rufiji, Pangani, Bagamoyo pamoja na Zanzibar huku shughuli zilizotekelezwa na mradi huo ni upandaji wa miti ya mikoko heka 1,250 ujenzi wa ukuta wa Kisiwa Panza-Pemba wa mita 40, ujenzi wa ukuta wa Pangani wa mita 950; ujenzi wa makinga bahari matano (5) yenye urefu wa mita 100.
Awali Dkt. Jafo ameeleza mafanikio katika miaka 60 ya muungano ikiwa ongezeko la shule za msingi na sekondari, Vituo vya kutolea huduma za afya ngazi zote, upatikanaji wa maji vijijini kutoka KM 1,360 mwaka 1961 hadi KM 11,966 mwaka 2022., ongezeko la chakula pamoja na mwenendo wa ukuaji wa uchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na msemaji mkuu wa serikali, Mobhare Matinyi amesema kuwa kupitia mikutano hio ya kuelekea miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waheshimiwa mawaziri ambao wanasimamia wizara zenye taasisi za muungano wanapata fursa kuja kuzungumza na watanzania kuelezea tulipotoka, tulipo na tunapokwenda pamoja na wataalam kutoka taasisi za muungano watapata fursa ya kupita katika vyombo mbalimbali vya habari kuelezea masuala mbalimbali ya muungano yanayofanywa na serikali.
“Baada ya Muungano wetu Aprili, 1964, watanzania tuliendelea kutafuta jina litakaloifaa nchi yetu, ilipofika mwezi Oktoba, jina Tanzania likazaliwa. Kabla ya hapo nchi ilijulikana kama Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,” ameeleza Matinyi.
Pia ameshukuru viongozi ambao ni waasisi wa Muungano, Hayati Mwl. Julius Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Aman Karume kwa kudumusha muungano na watanzania kujivunia Jamhuri ya Muungano pekee iliyofanikiwa katika bara la Afrika kwani nchi nyingine zilijaribu lakini hazikumudu.
No comments:
Post a Comment