Ferdinand Shayo ,Tanga
Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki (EAMCEF),umetoa Sh milioni 600 kila mwaka kwa mkoa wa Tanga kwa ajili ya miradi rafiki ikiwemo ya utengenezaji majiko banifu,ufugaji wa nyuki na samaki kwa wananchi wanaozunguka hifadhi za mazingira asilia ikiwemo ya Amani.
Fedha hizo zimetolewa kwa zaidi ya miaka 10 zikilenga kuwainua wananchi kiuchumi ili waache shughuli za uharibifu wa mazingira katika misitu na kuwa mabalozi wa uhifadhi katika hifadhi za mazingira asilia ikiwemo za Amani na Nilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake,Katibu tawala Msaidizi anayehusika na uzalishaji,mkoa wa Tanga,Mhandisi Emigidius Kasunzu,alisema wananchi wa vijiji vinavyozunguka maeneo hayo wamepatiwa miradi hiyo rafiki na wameweza kujiongezea kipato na kuendelea kuhifadhi mazingira.
“Mfuko umesaidia kupungzua madhara ya mabadiliko ya tabia nchi,uhifadhi na miradi mingi ambayo inawasaidia wananchi kupata kipato.Kuanzia mwaka 206 mkoa tunapata kila mwaka Sh 600milioni ambazo zinaenda moja kwa moja kwa wananchi,”alisema
“Kuna miradi kama upandaji miti,majiko banifu,ufugaji nyuki na imesaidia kupunguza umasikini kwa wananchi kwani miradi hiyo inachocheka kupunguza ukataji wa miti msituni na wananchi wameanzisha miradi ambayo inakuwa endelevu na inavutia wananchi wengine kuacha shughuli za uharibifu wa mazingira,”aliongeza
Kijiji cha Shebomeza,kilichopo Kata ya Amani ni miongoni mwa vijiji vilivyonufaika na miradi ikiwemo mradi wa hifadhi ya ardhi na maji shambani ambapo kwa kupitia wataalam wa kilimo,wananchi wa eneo hilo wamefundishwa kilimo cha makinga maji.
Mmoja wa wakulima hao,Zabibu Rajabu,alisema awali hawakuwa na elimu ya kilimo ambapo kwa sasa kilimo cha makinga maji kinasaidia kuzuia mmomonyoko wa udongo na kwa sasa wanaweza kupanda mazao mbalimbali ikiwemo mahindi,mananasi,miwa na parachichi.
“Nilikuwa sivuni mahindi ila kwa sasa navuna kwani mvua inapokuja maporomoko yanakuwa hayapo tena,maji yanapotoka juu yanaishia kwenye kingamaji yanapita kwenye mferejei hayaendi kwa kasi,tunapanda kama hivi nanasi kwenye kinga maji kwa matumizi ya nyumbani na kuuza,miwa nakula mweneywe nafanya biashara,”alisema
Mratibu wa Mfuko huo Kanda ya Kaskazini,Magreth Victor,alieleza kuwa vikundi vya wananchi vimekuwa vikipewa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi katika maeneo yao ili kujiongezea kipato na kupunguza kasi ya uvunaji rasilimali za misitu.
“Kutokana na mazingira vijiji vingi mashamba yake yako kwenye miinuko hivyo uzalishaji ukawa mdogo na ili kupunguza uharibifu kwenye msitu kwa sababu watu wanapata kipato kupitia kwenye mazao tukaona ni vema tukaja na teknolojia ya kilimo cha kuhifadhi ardhi na maji shambani ili waweze kuvuna mazao mengi zaidi na kupunguza uharibifu kwenye msitu,”alisema
Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Muheza na Mratibu wa mradi huo,Sylvester Mziray,alisema mradi huo ulianza mwaka 2016 na hadi sasa wakulima 120 kutoka vijiji vitatu wamenufaika na elimu ya kilimo hicho hasa ikizingatiwa mashamba yao yako kwenye milima.
Alisema kwa sasa wakulima wameelimishwa juu ya kilimo hicho kinachosaidia kuondoa mmomonyoko wa udongo kupitia makinga maji wanayoweka shambani na kuwa baadhi ya wakulima wamepewa mradi wa kilimo cha parachichi ili kujiongezea kipato.
No comments:
Post a Comment