Na Carlos Claudio, Dodoma.
Imeelezwa kuwa maandalizi ya kukabiliana na majanga ni hatua na mipango ambazo serikali na taasisi inaziweka ili kuleta manufaa kwa wananchi wake kujiandaa kukabiliana na milipuko ikiwa ni pamoja na shughuli kama vile kutengeneza njia ya mawasiliano ya mpango wa mwitikio, mafunzo ya utoaji chanjo pamoja kukabiliana na mlipuko wa majanga.
Hayo yameelezwa Machi 21,2024 jijini Dodoma na Afisa Program wa Elimu ya Afya na Mabadiliko ya Tabia Jamii, Grace Msemwa wakati wa MEDIA SCIENCE CAFÉ ambayo imewakutanisha waandishi wa habari na wataalamu mbalimbali.
Lengo la semina hiyo ni kuimarisha uwezo wa vyombo vya habari juu ya kuripoti chanjo na maandalizi ya kukabiliana na milipuko ya magonjwa nchini Tanzania.
Bi Msemwa amesema Tanzania ni mmoja ya nchi ambazo zimewahi kukabiliana na changamoto za milipuko ya magonjwa kama COVID 19 pamoja na virusi vya Marburg iliyotokea Kagera.
Pia ameelezea lengo kuu la maandalizi ya kukabiliana na majanga ni kulenga na kupunguza kasi ya magonjwa ya kuambukiza, kulinda afya ya umma na kudumisha huduma muhimu wakati wa hali ya dhoruba na endapo janga limetokea wizara hushirikiana na wadau ambao wanahusika katika kutoa majibu ya dharura, ajenda ya afya ya umma kwa ujumla.
“Somo ambalo tumelipata katika milipuko iliyotokea awali ni uchunguzi wa mapema na mwitikio wa haraka kwa mfano tukigudua hii jamii ina waathirika wa COVID 19 kuna timu ya wizara ya afya ya ufuatiliaji na epidemiolojia huwa wanaenda kwa ajili ya kufanya uchumguzi pale, kugundua tatizo na kuchukua vipimo kupeleka maabara na kama itagundulika kuna tatizo basi taratibu za haraka zitachukuliwa kwa wale waathirika wa lile eneo, lakini kingine ni ushirikiano wa kimataifa ikiwemo mataifa pamoja na taasisi zisizo za kiserikali,” amesema Msemwa.
Naye Bwana Richard Msittu kutoka SIKIKA amezungumzia umuhimu wa utoaji taarifa wakati wa mlipuko wa majanga pamoja na kuelezea ujumbe wa afya kwa umma na kusema kuwa mchakato mzima wa kuhabarisha na kusambaza taarifa sahihi kuhusiana na mlipuko husika au ugonjwa inatakiwa kufikia jamii kwa usahihi.
“Uandishi wa habari ni kama nyenzo ya serikali kuhakikisha kwamba taarifa sahihi inafikia jamii kubwa kwa upande wa serikali kuna watangazaji au watoaji wa taarifa za mwanzo ambapo kwa itifaki ya mawasiliano ya serikali maana yake waziri husika ndiye mwenye mamlaka ya kutangaza hali baada ya kujiridhisha na vipimo kutoka kwenye maabara za ndani au maabara za kitaifa kulingana na uwezo wa uchunguzi ambapo unaofanyika.”
Msittu amesema,“Katika muundo wa serikali kuna wasemaji katika ngazi tofauti tofauti ambao pia nao wana nafasi kubwa za kutoa matamko lakini hapa ndipo kwenye changamoto kidogo wale wasemaji kwa mfano ukichukulia mganga mkuu wa mkoa na mganga mkuu wa halmashauri lakini pia kuna mfawidhi wa hospitali ambapo kesi kwake imegudulika na taharuki imetokea, yeye anaweza kusema kitu gani? Lakini pia kuna mfawidi mpaka wa zahanati ambapo kwenye jamii kabla wizara kutuma timu anakuwa ameshakwenda kuchukua vipimo na kusoma ugonjwa, je yeye pia anasema nini? Kwaio kuna namna ya usemaji anaruhusiwa kusema kulingana na itifaki ya serikali lakini anasema nini? Mwandishi wa habari anatakiwa achukue namna gani ya habari kwa mtu yule?
Pia amesema wanahabari wanatakiwa wazingatie taarifa wanazozitoa kwa jamii kwani zinatakiwa ziendane na miongozo iliyowekwa na wizara ambayo itawalinda waandishi wa habari hasa katika kipindi cha mlipuko ili kuepusha usambazaji wa taarifa usio sahihi katika jamii.
Kwa upande wake meneja mikakati TAMWA, Sylvia Daulinge ameitaka jamii ibadilike na kuchukua hatua sahihi za kitaalamu na amesema kwa kuwa mabadiliko ni mchakato basi wana habari wanapaswa kuzingatia utoaji wa taarifa kuanzia taarifa inapotolewa na kuhakikisha ni nani anayetoa taarifa hiyo bila kusahau miongozo kwa wanahabari ni jambo la muhimu na ikifwatwa vizuri jamii itaenda kuelimika na kusaidiwa hasa sehemu zenye mikusanyiko kupitia mifumo na miongozo thabiti inapotokea milipuko.
No comments:
Post a Comment