REA YATUMIA BILIONI 44 KUJENGA MIRADI YA KUSAMBAZA UMEME VIJIJINI MKOANI PWANI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, March 19, 2024

REA YATUMIA BILIONI 44 KUJENGA MIRADI YA KUSAMBAZA UMEME VIJIJINI MKOANI PWANI


Zaidi ya shilingi bilioni 44.14 zimetumiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa ajili ya ujenzi wa Miradi ya kusambaza umeme ya vijijini katika mkoani Pwani ambapo katika vijiji 407 kati ya 417 vimenufaika kupitia Miradi nane (8) inayotekelezwa kwenye mkoa huo.

Miradi hiyo ni pamoja na REA I, REA II, REA III (Mzunguko wa Kwanza); Mradi wa Kusambaza Umeme kwenye maeneo ya Vijiji Miji (Peri Urban), Ujazilizi, Mradi wa Kusambaza Umeme kwenye maeneo ya Migodi na Shughuli za Kilimo, Mradi wa Kusambaza Umeme kwenye Visima vya maji na Vituo vya Afya (UVIKO 19) pamoja na Mradi wa REA III (Mzunguko wa Pili).

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA); Mhandisi, Hassan Saidy alisema hayo Tarehe 18 Machi, 2024 wakati akiongea mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Nishati na Madini walipotembelea kijiji cha Tukamisasa kilichopo tarafa ya Ubena Zomozi Halmashauri ya wilayani Chalinze mkoani Pwani kujionea maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa REA III (Mzunguko wa II).


Mhandisi Saidy alisema vijiji hivyo vilivyounganishwa umeme ni sawa na asilimia 96.4 ambapo vijiji 10 pekee ndivyo vilivyobaki vikiwa katika wilaya ya Mkuranga, Kibiti na Mafia na kwamba vitakamilika hivi karibuni kabla ya mwezi Juni, 2024 sababu mkandarasi anaendelea na kazi huku REA ikiwa tayari imeandaa mpango wa kuvipatia umeme wa nishati mbadala vijiji vyenye changamoto ya miundombinu ya mawasiliano.

“Vijiji vitano kati ya 10 vilivyopo maeneo ya Delta ya Rufiji vimetambuliwa kuwa vinapitika kwa njia ya barabara za msimu na vinaweza kuunganishwa umeme wa gridi, mkandarasi yupo maeneo ya Mradi ili kufanya tathmini ya njia ya kusambaza miundombinu ya umeme katika vijiji hivyo, kazi ambayo inatarajiwa kukamilika kabla ya tarehe 30 Juni mwaka huu”. Alisema Mhandisi, Saidy.


Hata hivyo alisema tayari mkandarasi wa Mradi mkubwa wa REA III (Mzunguko wa Pili) anayetekeleza Mradi huo kwa mkoa wa Pwani, Kampuni ya China Railway Construction Electrification Bureau Group (CRCEBG) ameshatekeleza mradi kwa wastani wa asilimia 99.5 huku akitarajiwa kukamilisha kazi hiyo, Machi 31 mwaka huu (2024). 
 
Aidha, Mhandisi Saidy alisema Mradi umelenga kupeleka umeme katika migodi midogo 30 iliyopo kwenye Wilaya za Bagamoyo, Chalinze na Kisarawe pamoja na maeneo ya kilimo ambayo hayajafikiwa na umeme mkoani Pwani kwa gharama zaidi ya shilingi Bilioni 2.456 ambapo mradi huo pia unatekelezwa zaidi ya mkoa wa Pwani kwa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 20.332. 
 
Hata hivyo, Mhandisi Saidy alisema kazi ya kupeleka umeme katika Kijiji cha Tukamisasa kilichopo Halimashauri ya wilayani Chalinze ilihusisha ujenzi wa njia za umeme wa msongo wa kati kwa kilomita 10.6, kilomita 3.3 za njia ya msongo mdogo na kufunga mashine umba 11 (Transformer) kazi ambazo zimekamilika kwa asilimia 100 na tayari Wateja wameshapatikana.
 
“Katika Kijiji hicho, Wateja 23 wa awali kati ya 66 walio katika wigo wa Mradi wameshaunganishiwa huduma ya umeme na zaidi ya shilingi milioni 466 zimetumika katika ujenzi wa miundombinu na kufikisha huduma ya umeme katika kijiji hicho”. Alisema, Mhandisi, Saidy.
 
Ameongeza kuwa tangu REA ianzishwe mwaka 2007 jumla ya vijiji 11,843 vimeunganishwa na nishati ya umeme ambayo ni sawa na asilimia 96 ambapo ni vijiji 475 tu ndiyo vimesalia na ameahidi kuwa hadi mwezi Juni mwaka huu vijiji hivyo vitakuwa vimeunganishwa na huduma ya umeme.
 
Alisema lengo la REA ni kukamilisha mpango wa Serikali wa kuhakikisha wanafikisha huduma ya umeme vijijini kwa asilimia kubwa kabla mwezi Juni, 2025.

Hata hivyo, aliahidi kusimamia utoaji elimu kwa Wananchi wa mkoa wa Pwani ili waongeze mwitikio na kuchangamkia fursa ya umeme kwenye maeneo yao na tofauti na ilivyo sasa ambapo mwitikio upo chini.
 
Naye Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga alisema Serikali inafanya mapitio ili kuja na viwango stahiki za gharama za kujiunga na huduma za umeme kwenye maeneo yenye sifa ya vijiji lakini yapo mijini ambapo Wabunge wengi walihoji kuhusu gharama za kujiunga na hudumaya umeme kati ya shilingi 27,000 (Vijijini) na shilingi 320,000 (Mijini).
 
Kapinga alisema wakazi wa vijijini hulipia shilingi 27,100 tu ambayo ni kodi baada ya serikali kulipia gharama zote huku wakazi wa vijiji miji wakilazimika kulipia shilingi 320,000 sawa na wakazi wa mijini.
 
“kwa mradi wa REA, Serikali hupipa kodi zote kwa asilimia 100 kwa kila mteja na hivyo mteja kulipia shilingi 27,100 pekee ya kuingiza umeme ambayo ni kodi ya asilimia 18 ya shilingi 150,000 aliyopaswa kulipa, lakini kwa malipo ya wateja wa vijiji miji na mijini hulipa wenyewe gharama zote za shilingi 320,000” alisema Kapinga.
 
Alisema mapitio hayo yatasaidia pia kuendelea kutolewa elimu kwa jamii ili kuwaongezea uelewa na mwitikio wa matumizi ya umeme nchini.
 
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Dkt. James Mataragio alitoa rai kwa Wananchi kuchangamkia fursa iliyopo mbele yao kwa sasa ya kujiunga na huduma ya umeme kwenye makazi yao yao jambo litakaloiletea Serikali maana matumizi makubwa ya fedha kwenye Miradi ya hiyo ambapo lengo ni umeme kufika kwa kila Mwananchi hususan maeneo ya vijijini. 
 
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Nishati na Madini, Dkt. Mathayo David Mathayo aliwashauri wakazi wa vijijini kuona umuhimu wa matumizi ya nishati ya umeme kwa maendeleo yao kwa kuuza kuku wawili ili kujiunga na huduma ya umeme badala ya kisingizio cha kukosa fedha ya kwa kuwa fursa imesogezwa na Serikali kwenye makazi yao.
 
Naye Habiba Athumani mkazi wa kijiji cha Tukamisasa aliishukuru Serikali kwa kuwaingizia umeme na kuomba huduma ya upatikanaji wa umeme kwa wepesi ili iende sambamba na upatikanaji wa maji na kuwaepusha na adha ya magonjwa ya milipuko kutokana na kutumia maji yasiyo safi na salama.
 
Naye Shabani Tungo, mkazi wa Kijiji hicho alishukuru Serikali kwa kuwafikishia huduma ya umeme ambayo inaonekana kurahisisha shughuli zao za kiuchumi kwa kufungua biashara mbalimbali zinazo waingizia kipato ikiwemo “Saloon” za kike na za kiume na mashine za kusaga nafaka.

No comments:

Post a Comment