TANZANIA YAADHIMISHA SIKU YA UNYANYAPAA DUNIANI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, March 19, 2024

TANZANIA YAADHIMISHA SIKU YA UNYANYAPAA DUNIANI.


Na Okuly Julius-Dodoma 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe Jenista Mhagama amesema lengo la maadhimisho ya Siku ya Unyanyapaa na Ubaguzi Duniani ni kukumbushana wajibu wa kila mmoja wetu, taasisi na asasi mbalimbali  kwa ajili ya  kupaza sauti na hivyo kupinga na kupiga marufuku vitendo vyote vya unyanyapaa na  Ubaguzi na kukosekana  usawa na haki miongoni mwa makundi mbalimbali ya kijamii.



 Hayo yamesemwa leo kwenye hotuba yake iliyosomwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt Jerome Kamwela.


Amesema dhana na vitendo vya Ubaguzi vinavyoashiria kutokuwepo kwa usawa vinasababisha kutotimia kwa malengo yetu ya kitaifa ya mwitikio wa VVU na UKIMWI na kurudisha nyuma jitihada za Serikali za kutokomeza UKIMWI.


Maadhimisho hayo yalibebwa na kauli mbiu isemayo Linda

 Afya kwa kulinda haki” inahimiza  kuwa na mifumo imara ya kisheria, kiutamaduni na kijamii ili kujenga mazingira yanayopelekea uwepo wa haki katika upatikanaji na  utoaji huduma bora za kiafya. 


Aidha amesema kauli mbiu hii inatutaka kuimarisha  mifumo yetu  kwa ajili ya kuweka  usawa na kutokomeza  ubaguzi na unyanyapaa miongoni mwa watu wanaoishi na VVU. 


Mwenyekiti wa Baraza la Watu wanaoishi na VVU (NACOPHA) Bibi Leticia Moris amesema Unyanyapaa na ubaguzi bado upo na unatishia mwamko wa jamii kutumia huduma za UKIMWI zinazotolewa na Serikali na kwa gharama kubwa na hivyo kurudisha nyuma jitihada za Serikali na wadau katika kutokomeza VVU na UKIMWI nchini. 


Bi Leticia ametaja Mila potofu, imani za kidini, uelewa mdogo juu ya UKIMWI ni baadhi ya vichocheo vya unyanyapaa katika jamii zetu.


Aidha amesema kuwa kupitia ufadhili wa wadau mbalimbali wa maendeleo, Baraza linatekeleza shughuli za mwitikio wa UKIMWI ikiwa ni hatua za kuunga mkono jitihada za Serikali kufikia malengo ya 95-95-95 ifikapo 2030. 


Bi Leticia ameongeza kuwa katika jitihada za kupinga unyanyapaa na ubaguzi kwa WAVIU, moja ya vipaumbele vya Baraza ni kujenga uwezo wa WAVIU katika makundi mbalimbali ngazi ya jamii, ambapo kwa sasa  baraza linaratibu Mitandao ya Kitaifa mitatu   kwa lengo la kuongeza wigo wa ufikiwaji wa makundi hayo katika huduma za VVU na UKIMWI, kupunguza athari za unyanyapaa na ubaguzi miongoni mwao, na kuhimiza kudumu katika ufuasi sahihi wa dawa za kufubaza VVU.


 Ameyataja makundi hayo kuwa ni Watu wenye Ulemavu, Wanawake na Vijana, yaani; Mtandao wa Kitaifa wa Watu wenye Ulemavu wanaoishi na VVU (NNPD+), Mtandao wa Kitaifa wa Wanawake Wanaoishi na VVU (NNW+), na Mtandao wa Kitaifa wa Vijana wanaoishi na VVU (NYP+).


Mkurugenzi Mkazi wa UNAIDS Bw. Martin Odiit amesema suala la unyanyapaa na ubaguzi ni ukiukwaji wa haki za binadamu na hivyo hauhitaji kuendelea kuwepo kwakuwa unarudisha nyuma mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.


Dkt Odiit ameongeza kuwa kuna makundi mengi yanayoathiriwa na unyanyapaa na ubaguzi yakiwemo makundi ya vijana hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha tunamaliza unyanyapaa.


Aidha ameongeza kuwa UNAIDS itaendelea kutoa  ushirikiano katika kuhakikisha unyanyapaa na ubaguzi unamalizika.








No comments:

Post a Comment